• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Raia wa kigeni aliyefariki alikuwa amejidunga kokeni – Polisi

Raia wa kigeni aliyefariki alikuwa amejidunga kokeni – Polisi

MOHAMED AHMED na FARHIYA HUSSEIN

RAIA wa Austria ambaye aliaga dunia Jumatano iliyopita baada ya kuanguka kwenye klabu eneo la Mtwapa, Kaunti ya Kilifi alikuwa amejidunga dawa za kulevya, taarifa ya polisi imebaini.

Armin Roeseler, mwenye umri wa miaka 47 alizirai katika klabu ya Casuariana ambapo yeye na rafikiye walikuwa wameenda kujiburudisha.

Aliaga dunia baada ya kukimbizwa katika hospitali ya Jocham, Kaunti ya Mombasa.

Afisa mkuu anayesimamia uchunguzi wa kisa hicho alisema Bw Roeseler alikuwa amejidunga dawa za kulevya aina ya kokeni.

Kulingana na polisi, jamaa huyo alijidunga katika mkono wake na ukaguzi wa mwili uliofanywa katika hospitali ya Jocham ulionyesha kuwa dawa hizo zilimdhuru.

Wakati huo huo, ripoti zilizotolewa na mashahidi zilieleza kuwa dakika chache baada ya jamaa huyo kuingia kwenye klabu alionekana akiwauliza wanawake wawili, Everylne Chengetich na Lydia ambao wamekamatwa na polisi ni wapi angeweza kupata kokeni.

Shahidi ambaye tunabana jina lake aliambia Taifa Leo kuwa mwendazake pamoja na mtalii mwingine walionekana wakiingia katika klabu hiyo pamoja na wanawake hao wawili muda wa saa saba usiku Jumanne.

“Wanawake hao hawakuweza kumsaidia lakini walimwelekeza kwa dereva wa teksi ambaye alimletea dawa hizo baada ya kumpa Sh10,000,” taarifa ya polisi ilisoma.

Baada ya kujidunga dawa hizo alionekana akienda msalani kila wakati.

“Iliripotiwa kuwa jamaa huyo alianguka ghafla na kukimbizwa katika hospitali ya Jocham,” akasema afisa mkuu wa Kaunti ya Kilifi, Esau Ochorokodi.

You can share this post!

Maharamia wakata mkazi kichwa

WANDERI: Kanisa lisiwe mateka wa wanasiasa nchini

adminleo