MATHEKA: Viongozi wa makanisa wawazime wanasiasa
Na BENSON MATHEKA
Vurumai zilizotokea katika kanisa la Gitui, Kaunti ya Murang’a mnamo Jumapili ambapo wanasiasa wa makundi mawili yanayozozana katika chama tawala cha Jubilee yalikabiliana zinatokana na viongozi wa kidini kukataa ushauri.
Mara kwa mara, wito umekuwa ukitolewa kwa viongozi wa makanisa kukoma kuwaruhusu wanasiasa kutumia makanisa kuendeleza ajenda zao.
Wamekaidi ushauri huo na kuendelea kualika wanasiasa kuchanga pesa katika makanisa yao.
Hii ni baada ya pesa ambazo baadhi ya wanasiasa wanatoa kwenye michango hiyo kushukiwa kuwa mapato ya ufisadi.? Licha ya kushauriwa wasichangamkie pesa kutoka kwa wanasiasa, imekuwa ni kama kupigia mbuzi gitaa.
Wameendelea kuwakambutia wanasiasa ambao wanatoa michango minono na kusahau jukumu lao la kutoa ushauri wa kiroho kwa watu.
Vurumai za Jumapili katika kanisa hilo hazingetokea kama wanasiasa hawangekuwemo.
Na ikiwa hawatakoma kualika wanasiasa yaliyoshuhudiwa katika kanisa hilo ni mwanzo tu. Nasema hivi kwa sababu joto la kisiasa linaendelea kupanda nchini kufuatia juhudi za kubadilisha katiba huku uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.
Wanasiasa nao wamegundua kuwa ni makanisani wanakoweza kupata watu wakiwa wamekusanyika ili kuwauzia sera zao bila kutumia gharama yoyote.
Hii ndiyo sababu kila Jumapili wanasiasa wamekuwa wakihudhuria ibada kwa makundi na kushambulia wapinzani wao.
Viongozi wa kidini wanapaswa kujua kuwa wanaweka nchi katika hatari kubwa kwa kuruhusu wanasiasa kutumia makanisa kuwa majukwaa ya kulaumiana.
Nashawishika kusema kuwa tamaa ya viongozi wa kidini ya kupenda pesa na kuwasifu wanasiasa wanaowapa donge bila kuuliza wanakotoa pesa hizo inaweza kuchoma nchi hii.
Viongozi wa kidini wanafaa kukosoa wanasiasa jambo ambalo ni mlima katika mazingira ya sasa nchini kwa sababu kupitia michango, wanasiasa wamewaweka chini ya himaya zao.
Ninaamini kuwa viongozi wa kidini wana haki ya kujiunga na vyama vya kisiasa kama raia wengine lakini sikubaliani nao wanaporuhusu wanasiasa kubadilisha maeneo ya ibada kuwa kumbi za kuandaa mikutano ya kisiasa au kutumia makanisa kupigia debe wanasiasa.
Kufanya hivi kuna hatari ya kufanya dini kupoteza maana yake kabisa na hali kuwa mbaya zaidi.
Viongozi wa kidini wanapaswa kuwa wapatanishi mgogoro unapozuka kati ya wanasiasa na katika hali ya sasa, ni vigumu kutekeleza jukumu hilo bila kupendelea upande wowote.
Ni viongozi wa kidini pekee wanaoweza kukomesha wanasiasa kwa kuwanyima nafasi ya kuhutubu katika makanisa yao.
Sidhani kuna dini inayofunza viongozi kutambua wanasiasa wakihudhuria ibada na kuwapa nafasi ya kuhutubia waumini.
Mwai Kibaki alipokuwa rais, alikuwa akihudhuria ibada katika makanisa jijini Nairobi na mjini Nyeri na hakuwa akihutubia waumini.
Ikiwa viongozi wa kidini na hasa makanisa wanataka kulinda hadhi ya sehemu za ibada wanafaa kupiga marufuku wanasiasa.
Wawachukulie kama waumini wengine wanapohudhuria ibada na iwapo ni lazima wahutubu, isiwe ni kutoa matamshi ya uchochezi.
Muhimu kabisa ni kuepuka kualika makundi ya wanasiasa kuendeleza ajenda za mirengo yao kwa kisingizio cha kufanya harambee.