• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
GWIJI WA WIKI: Mutwiri Wanjagi

GWIJI WA WIKI: Mutwiri Wanjagi

Na CHRIS ADUNGO

MBALI na kuwa johari adhimu na kito adimu chenye thamani kubwa maishani mwa kila mpenzi na mtetezi mfia-lugha, Kiswahili kinalipa sana hasa kwa wale wanaojitolea sabili kukitumikia kikamilifu.

Mafao ya Kiswahili yatabakia kuwa mengi na yasiyo na kifani kwa kila anayeipenda lugha hiyo.

Pania mno kuongozwa na mapenzi ya dhati katika chochote unachokifanya huku ukijiweka huru kutembea na waliofanikiwa katika nyanja unazozizamia ili nao wakushauri zaidi, wakuchochee sana na kukuelekeza ipasavyo katika kila hatua.

Huu ndio ushauri wa Bw James Wanjagi Mutwiri -mwalimu mbobevu, mwandishi chipukizi wa Fasihi Pendwa na mtaalamu wa ushairi ambaye kwa sasa anafundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Chogoria Boys, Kaunti ya Meru.

MAISHA YA AWALI

Mwalimu Mutwiri ndiye mziwanda katika familia ya watoto saba wa Mzee David Njagi na Bi Beterine Thereru.

Alizaliwa zaidi ya miongo mitatu iliyopita kijijini Ereani, eneo la Chuka, Wilaya ya Meru Kusini katika Kaunti ya Tharaka-Nithi. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Chuka DEB kati ya 1986-1994 na kuibuka mwanafunzi bora Wilayani alipokwangura alama 525 kwa 700 katika mtihani wa KCPE mwishoni mwa 1994.

Alijiunga na Shule ya Upili ya Ndagani Mixed mnamo 1995 na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 1999. Mutwiri alikuwa miongoni mwa wanafunzi watatu bora waliotokea Ndagani Mixed na kuingia chuo kikuu baada ya kufaulu vyema zaidi mtihanini na kuletea shule yao sifa sufufu.

Kutoka pale, alijiunga na Chuo Kikuu cha Laikipia, kusomea ualimu akizamia sana Kiswahili na somo la Dini kati ya 2001 na 2005. Huko, alifundishwa na wahadhiri mahiri waliompa kila sababu ya kukichapukia Kiswahili bila ya kukionea aibu.

Dkt Sheila PAM Wandera alimfaa pakubwa katika suala la kujiendeleza kitaaluma na kumpokeza malezi bora zaidi hasa katika ulingo wa sanaa ya utunzi wa mashairi.

Kufikia sasa, Mutwiri amechangia zaidi ya mashairi 2,500 katika kurasa za Ushairi wa Kiswahili zinazochapishwa na gazeti la Taifa Leo kila wikendi na Jumatatu.

Walimu waliomfundisha Mutwiri akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi na upili walitambua mapema ukwasi wa kipaji cha mwanafunzi wao huyu katika utunzi wa mashairi ya Kiswahili kutokana na upekee wa umilisi wake wa lugha.

UALIMU

Kabla ya kuhitimu chuoni, Mutwiri aliwahi kufundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Wise Dove akiwa mwalimu wa msimu. Aliaminiwa kuwanoa wanafunzi wa darasa la sita na saba shuleni humo.

Baada ya kufuzu mnamo 2006, alishika chaki katika Shule ya St Pauls Mariani akiwa Mkuu wa somo la Kiswahili na Naibu Mwalimu Mkuu.

Mnamo 2007, alipata uhamisho hadi Kieni Girls, Embu alikoamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake idarani.

Alihudumu huko kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuhamia rasmi katika Shule ya Kitaifa ya Chogoria Boys, Kaunti ya Meru mnamo 2008.

Huko ndiko anakojipatia riziki yake mpaka leo. Akiwa kwa sasa Mkuu wa Idara ya Kiswahili, Bw Mutwiri pia ni mtunzi na mtahini wa kitaifa wa KCSE Kiswahili hasa Karatasi ya Kwanza (Insha) na Karatasi ya Pili (Sarufi na Matumizi ya Lugha).

Mnamo 2008, alijiunga na Chuo Kikuu cha Chuka kusomea Shahada ya Uzamili katika Fasihi, akijikita zaidi katika fani ya ushairi chini ya usimamizi na uelekezi wa Bw Enock Matundura, Bw Mugambi Bita na Profesa John Kobia waliomsaidia pakubwa kuandaa na kuwasilisha tasnifu yake.

Hamu ya Mutwiri ya kuzamia Kiswahili chuoni ni zao la kutangamana kwake kwa karibu mno na baadhi ya wanafunzi wenzake waliomwamshia ujasiri wa kukiasisi Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka (CHAKICHU).

Akiwa mtahini mwenye tajriba pevu na uzoefu mpana katika Insha na Sarufi ya Kiswahili, Mutwiri anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuwaelekeza, kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya KCSE Kiswahili.

Anakiri kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili Shuleni Chogoria Boys, ni nguzo kubwa katika ufanisi wapatao kila mwaka matokeo ya KCSE yanapotangazwa.

Mnamo 2018, Kiswahili kilikuwa miongoni mwa masomo yaliyofanywa vyema zaidi na watahiniwa wa KCSE kutoka Chogoria Boys. Awali katika mwaka wa 2017, watahiniwa wa shule hii walikuwa wamejizolea alama wastani ya 9.5 katika KCSE Kiswahili.

Tangu mwaka wa 2008, Kiswahili kimekuwa kikiibuka bora Shuleni Chogoria Boys kati ya masomo yote ya lazima yanayotahiniwa katika KCSE.

Akipania kuvumisha zaidi matokeo ya Kiswahili mwaka huu wa 2019, Mutwiri analenga kuwachochea wanafunzi wake kusajili alama wastani ya 10.5 katika KCSE Kiswahili.

UANDISHI

Mnamo 2016, shirika la Huduma za Kielimu kwa Taifa (NES) lilimfyatulia Mutwiri diwani ‘Miale ya Mashairi’. Akishirikiana na Bi Maria Mvati na Bw James Kanuri (wahariri), Mutwiri alichangia mashairi 10 ya bahari ya kikwamba katika diwani hiyo.

Kitabu chake cha pili ni ‘Uchambuzi wa Mashairi na Maswali: Ladha ya Lugha’ alichojichapishia mnamo 2016. Baada ya kampuni ya Bookmark Publishers kumtolea kitabu ‘Tunu ya Lugha: Mitihani ya Karatasi ya Pili na Tatu’ mnamo 2017, Mutwiri alichapisha kitabu ‘Utamu wa Ushairi’ ambacho kina jumla ya tungo 60 za mashairi yake.

Ametunga idadi kubwa ya hadithi fupi na mashairi ambayo yamewahi kuchapishwa katika gazeti la Taifa Leo na kufana sana katika tamasha za kitaifa za muziki tangu 2017.

Kitabu chake ‘Mwanga wa Fasihi’ kinachorejelea mashairi yake yote yaliyowahi kutumiwa katika tamasha za muziki kote nchini kuanzia 2017, kinatazamiwa kutolewa na kampuni ya Micharazo Publishers hivi karibuni. Kwa kushirikiana na walimu wengine wanaofundisha katika shule mbalimbali za upili kutoka humu nchini, Mutwiri kwa sasa anaandaa diwani ‘Utenzi wa Bara’ kwa matarajio kwamba itachapishwa hivi karibuni.

FAHARI

Mutwiri anajivunia kuchangia na kushiriki uendeshaji wa vipindi vya lugha katika takriban runinga na redio zote za humu nchini. Kila wikendi, angejumuika na wanafunzi wake kusikiliza vilivyokuwa vipindi ‘Kamusi ya Changamka’ (Qfm na Qtv) na ‘Bahari ya Lugha’ (Radio Citizen).

Nyakati za vipindi hivyo vya lugha, angewahimiza wanafunzi wake kuwasikiliza kwa makini mikota wa lugha walioaminiwa kudadavua masuala mbalimbali yahusuyo Kiswahili kwa weledi mkubwa ajabu. Mbali na kuchangia kwa ujasiri uendeshaji wa vipindi ‘Ramani ya Lugha’ (KBC Idhaa ya Taifa) na ‘Nuru ya Lugha’ (Radio Maisha), Mutwiri anajivunia pia kuchangia pakubwa mafundisho ya Kiswahili kupitia tovuti ya swahilihub.com.

Kwa pamoja na mkewe Bi Cecilia Muthoni ambaye ni mwanamitindo na mfanyabiashara, Bw Mutwiri amejaliwa watoto wawili – Nashlya Makena na Vivian Mutugi ambao wamepania kuzifuata nyayo za baba yao kwa kasi ya duma.

You can share this post!

Trump ampiga kalamu mshauri wa masuala ya usalama

WASIA: Yakome mahusiano ya kiholela hata yawe na mikataba...

adminleo