• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
SEKTA YA ELIMU: Wanachekechea nao wafumbatwe katika mpango wa elimu bila malipo

SEKTA YA ELIMU: Wanachekechea nao wafumbatwe katika mpango wa elimu bila malipo

Na CHARLES WASONGA

NI haki ya kila mtoto nchini kupata elimu ya msingi bila malipo, na ya lazima, kulingana na kipengee cha 53 (1) (b) cha Katiba ya sasa.

Haki hiyo pia inatetewa katika Sheria ya Elimu ya Msingi ya 2013.

Lakini kinaya ni kwamba haki hii imekuwa ikitolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na wale wa shule za upili pekee huku shule za chekechea zikisazwa.

Hii ndio maana wadau katika sekta ya elimu wamechangamkia mswada ambao unalenga kulazimisha serikali za kaunti kutoa elimu ya chekechea bila malipo kwa watoto chini ya umri wa miaka sita ikiwa mswada ulioko bungeni wakati huu utapitishwa na kuwa sheria.

Mswada wa Masomo ya Chekechea wa 2018 unalenga kufutilia mbali karo ambazo watoto wa kati ya miaka mitatu na mitano hutozwa katika shule za nasari za umma.

Pendekezo hilo linajiri miaka 16 baada ya serikali ya kitaifa kuanza kutekeleza Mpango wa Elimu bila Malipo katika shule za msingi za umma kote nchini kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu ya msingi.

Kando na hayo mswada huo unaunda sheria mahsusi ambao utatumiwa kusimamia shule zote za chekechea kote nchini. Hii ni kwa sababu wakati huu hakuna sheria inayotumiwa kuendesha shughuli katika shule hizo ambazo hutoa elimu ya msingi kwa watoto.

“Katika juhudi za kulinda na kukuza haki ya mtoto kupata elimu ya msingi, kila kaunti itahitajika kutoa elimu bila malipo na ya lazima katika shule zote za umma katika kaunti husika,” mswada huo unasema.

Mswada huo pia unahitaji kwamba wale wanaohudumu kama walimu wa shule za chekechea angalau wawe wamehitimu kwa kupata cheti cha diploma kutoka vyuo vya mafunzi ya walimu wa chekechea.

Aidha walimu hao sharti wawe wamesajiliwa rasmi na Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC).

Vilevile, mswada huo, ambao umedhaminiwa na Seneta wa Bomet Christopher Langat, anapiga marufuku matumizi ya aina yoyote ya mitihani kama kigezo cha kuwezesha mwafunzi kusajiliwa katika shule za chekechea au kumwezesha kujiunga na darasa la juu.

“Shule ya chekechekea chini ya sheria hii haitaruhusiwa kuwatahini watoto kwa ajili ya kusajiliwa kwayo,” mswada huo unasema.

Ufaafu

Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi (KPA) Nichalas Maiyo ameikaribisha sheria hiyo akisema itawafa zaidi watoto kutoka jamii zenye mapato ya chini kupata msingo bora wa elimu.

“Watoto wengi kutoka jamii masikini huwa hawapati nafasi ya kupata elimu ya chekechea kwa sababu ya wazazi wao hushindwa kumudu gharama ya karo. Sheria hii imejiri wakati mzuri kwani baadhi ya shule za chekechea hasa zile za binafsi hutoza karo ya hadi Sh80,000 kwa mwaka. Na hii ndio maana wazazi wengi kupeleka watoto wao katika shule za umma ambazo pia hutoza karo,” anasema.

Bw Maiyo pia anafurahi hitaji kuhusu utihimu wa walimu wa chechekea akisema na kusajiliwa kwao na TSC kwamba hatua hiyo itaboresha viwango vya masomo katika shule hizo.

Kuna zaidi ya shule 40,000 za chekechea kote nchini, na takriban asilimia 70 kati yazo ziko ndani ya shule za msingi. Na kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) idadi ya walimu katika shule hizo ni zaidi ya 160,000.

You can share this post!

USWAHILINI: Matumizi kedekede ya udi miongoni mwa jamii za...

SAUTI YA MKEREKETWA: Eti kumkomboa Mwafrika? Ndoto tupu za...

adminleo