SAUTI YA MKEREKETWA: Eti kumkomboa Mwafrika? Ndoto tupu za alinacha!
Na HENRY INDINDI
NITANGULIZE kwa kutangaza masikitiko makubwa kwa uanaharakati angamizi ambao hushuhudiwa Afrika Kusini kutokana na ubaguzi.
Yaani wanachodhihirisha raia hawa wa Afrika Kusini ni kwamba kumkomboa Mwafrika si jambo rahisi maanake mwenyewe hajithamini wala hamthamani Mwafrika mwenzake.
Hilo la kutojithamini yeye na amali zake ndilo husababisha kutomthamini mwenzake.
Mwafrika anayejiona kuwa duni ni rahisi sana kwake kufikiri kwamba ‘uduni’ wake unatokana na kukandamizwa na wengine ilhali mwenyewe anakosa kupiga hatua ya kuikomboa nafsi yake. Anataka kupewa, anataka kufikiriwa, na atake tena kufanyiwa.
Kutojithamini huku kwa Mwafrika ni dhahiri si Afrika Kusini tu bali kote kote barani.
Ukitaka kujua kwamba hujithamini, jiulize ni mara ngapi umeonea fahari kujitambulisha kwa jina lako la kiafrika badala ya hilo la kigeni ulilopewa.
Jiulize pia kuhusu vyakula unavyoonea fahari kula kisha utathmini ikiwa shibe ya vyakula hivyo inakuimarisha au inakumaliza.
Juzi tukitazama televisheni moja ya humu nchini, wenzangu tuliokuwa nao waliajabia kumwona mzungu akizungumza Kiswahili sanifu na vizuri sana. Walikiri kwamba alikuwa anazungumza Kiswahili kizuri kuwashinda.
Nilipowaambia kwamba alikuwa Dunford yule mwogeleaji wa Kenya, walijiajabia hata zaidi.
Kustaajabu kwao kulinikumbusha kongamano la kibiashara tuliloshiriki majuzi na ndugu yangu Mwalimu Andrew Watuha.
Lilikuwa kongamano la kimataifa kwa hivyo lilikuwa na raia wa kutoka kotekote ulimwenguni. Katika kongamano hili kulikuwa na mambo mawili yaliyonigusa na kunipa sababu zaidi za kumwajabia Mwafrika na kutojithamini kwake.
Kwanza, kuna mwanadada wa asili ya Kirusi aliyewasalimu washiriki katika Kiswahili kisha akatoa sentensi kadhaa za kuwajulia hali katika Kiswahili.
Badala ya kumjibu kwa furaha na kuonea fahari, kwanza Wakenya hawa waliangua kicheko kisha wengine wakajibu kwa kubambanya na wengine kumjibu katika Kiingereza. Ukereketwa wangu uliniwashawishi kuudhika lakini nikakumbuka kwamba hawa ni Waafrika. Hawajithamini.
Mwaliko
Kioja cha pili kilikuwa katika mwaliko wa karamu ya chakula cha jioni.
Mfawidhi alitangaza kwamba mavazi ya karamu hiyo yawe ya Kiafrika. Kwa hivyo nilitarajia kuona vitenge, vikoi au chochote cha kudhihirisha Uafrika hata kama ni shuka za Kimaasai.
Wakati wa karamu, ni watu wa kuhesabu tu waliofika karamuni na mavazi haya ya Kiafrika. Hili liliniwangisha kichwa.
Huyu Mwafrika atajithamini lini? Inaeleweka kwamba Kenya iliwahi kuwa na ndoto ya kuwa na vazi la kitaifa lakini ndoto hiyo ilibaki ndoto. Bado tunaendelea kuiota. Lakini hata tungefanikiwa kuwa na vazi hilo la taifa, tungelionea fahari gani ikiwa lugha ya taifa haijapata kuonewa fahari hiyo?
Matukio haya mawili yalikuwa fursa nzuri sana kwa Kenya kujidhihirisha kwa ulimwengu kama taifa linalojielewa na kujithamini lakini iliyoyomea huko katika upepo wa pwani. Inasikitisha.
Ninapoyaona haya ya Afrika Kusini, na kuyaunganisha na visa hivi nilivyoshuhudia katika kongamano, ninamsikitikia sana Mwafrika.
Kila mara Mwafrika huifanya hatua ya kujikomboa kwake kuonekana kama jambo lisilowezekana. Anapoendelea kutojithamini yeye na amali zake, inakuwa rahisi kupendekeza kwamba ni afadhali aendelee kuwatawaliwa. Inatamanisha hata kumkumbusha huyu mwafrika kwamba uhuru anaojidai kupata ni ndoto tu.