WAZITO WA ULAYA: Manchester City ina kikosi cha wanasoka ghali zaidi
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
KLABU ya Manchester City ndiyo iliyo na kikosi cha wanasoka ghali zaidi barani Ulaya, ripoti ya shirika la CIES Football Observatory imesema.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambao mnamo 2008 walinunuliwa na kampuni tajiri ya Abu Dhabi United Group, wametumia kiasi cha hadi Sh135.9 bilioni kupata wachezaji wao wa sasa.
Miamba hao wa Uingereza walimwaga sokoni kiasi mara 32 ya pesa zilizotumiwa na klabu za Norwich City kukisuka kikosi chao cha sasa kinachoshiriki Ligi Kuu ya EPL, ripoti hiyo imefichua.
Katika nafasi ya pili ni wapambe wa soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) Paris Saint-Germain (PSG) waliotumia takriban Sh110.4 bilioni kununua wachezaji wapya katika misimu ya hivi karibuni. Wanafuatwa na Real Madrid ya Uhispania (103.2 bilioni), huku Manchester United wakiweka mezani zaidi ya Sh85.9 bilioni kujisuka upya.
Katika utafiti wake, CIES ambayo makao yake yako nchini Uswizi, ilichunguza kwa makini uzoefu wa wachezaji zaji kwenye ligi tano kubwa za bara Ulaya; yaani EPL, La Liga (Uhispania), Serie A (Italia), Bundesliga (Ujerumani)na Ligue 1 kuanzia mwaka wa 2010.
Chelsea, Juventus, Atletico Madrid pamoja na Liverpool pia zimesemekana kuwa kwenye orodha ya timu zilizotumia kiasi kikubwa zaidi cha pesa ili kuvutia huduma za wachezaji wengi wa haiba kubwa kati ya mwaka wa 2010 na 2019.
Klabu ya AS Monaco nchini Ufaransa ndiyo iliyopokea kiasi kikubwa zaidi cha pesa baada ya kumuuza mvamizi chipukizi Kylian Mbappe aliyejiunga na PSG kwa kima cha Sh19 bilioni.
Klabu ya Lille ya Ufaransa iliongoza katika matumizi bora ya fedha kutokana na uhamisho wa baadhi ya wachezaji, ikifuatiwa na Monaco, Genoa, Olympique Lyon na Udinese.
Paderborn ya Ujerumani iliyopanda daraja msimu uliopita kushiriki kivumbi cha Bundesliga ilipatikana kuwa timu dhaifu zaidi kwenye orodha hiyo ya gharama ya matumizi baada ya kutumia kiasi kidogo zaidi cha fedha kusajili wachezaji wapya.
Man-City ambao walitwaa jumla ya mataji matatu msimu uliopita, walivunja rekodi yao ya usajili mapema mwaka huu walipolipa takriban Sh9.5 bilioni kujinasia maarifa ya kiungo Rodri kutoka Atletico Madrid. Kikosi chao cha sasa kinajumuisha wanasoka matata zaidi akiwemo David Silva ambaye alinunuliwa mnamo 2010.
Orodha ya timu 10 za kwanza:
1. Manchester City
2. Paris St-Germain (PSG)
3. Real Madrid
4. Manchester United
5. Juventus
6. Barcelona
7. Liverpool
8. Chelsea
9. Atletico Madrid
10. Arsenal
Timu nyingine zilizochaguliwa:
11. Everton
12. Tottenham Hotspur
19. Leicester City
21. West Ham United