• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
ANJELLA NANCIE: Walidhani nitakuwa mwanasayansi lakini natamba kwa uigizaji

ANJELLA NANCIE: Walidhani nitakuwa mwanasayansi lakini natamba kwa uigizaji

Na JOHN KIMWERE

AKIWA mdogo alitamani kuhitimu kuwa daktari wa upasuaji, lakini kwa sasa ni miongoni mwa wasanii wa kike wanaovumisha tasnia ya uigizaji nchini.

Hata hivyo analenga kuhitimu kwa shahada ya uzamili kwenye masuala ya uzalishaji (uprodyuza) katika chuo kimoja nchini Marekani.

Bi Anjella Nancie anasema kabla ya kujiunga na usanii, wengi walidhania angekuwa mwanasayansi, daktari au mtangazaji wa redio au Televisheni.

”Kwa wanamaigizo wa kimataifa nimepania nijitume zaidi nihakikishe nimefikia viwango vya wasanii shupavu kama Eva Longoria na Megan Markle wa Marekani na Uingereza mtawalia,” alisema na kuongeza kuwa anaamini hakuna kisichowezekana kwa kumwamini Mungu.

Pia anasisitiza kuwa angependa kushiriki uigizaji hadi atinge upeo wa kimataifa maana hakuna asiyependa maendeleo katika taaluma yake. Vile vile anataka kufikia viwango vya Mkenya mwenzake, Lupita Nyong’o anayetesa katika filamu za Hollywood.

Kwenye utangulizi wake alitua jijini Nairobi mwaka 2006 ambapo alibahatika kujiunga na kundi la Jicho Four Productions walipokuwa wakizalisha michezo ya kuigiza kupitia mwongozo wa vitabu za riwaya.

Anasema walikuwa wakionyesha (stage play) kwenye shule za upili mbalimbali nchini hali iliyompa nafasi kuzuru maeneo tofauti isipokuwa Mandera na Garisa.

Mwigizaji Anjella Nancie anayelenga kufikia upeo wa kimataifa miaka ijayo. Picha/ John Kimwere

Binti huyu anasema mwaka 2009 kimiujiza alibahatika kuigiza kwenye kipindi cha Papa Shirandula ndani ya muda wa miaka miwili pia kipindi cha Inspekta Mwala.

Papa Shirandula na Inspekta Mwala ambazo hupeperushwa kupitia Citizen Televisheni ni kati ya vipindi maarufu vilivyo na wafuasi wengi tu wapenzi wa burudani ya maigizo hapa nchini.

Tangu mwaka 2016 hadi sasa anashiriki kipindi kiitwacho ‘Kenda Imani’ ambacho hupeperushwa kupitia KCB Televisheni. Pia anashiriki filamu ya ‘Varshita’ ambayo huonyeshwa kupitia Maisha Magic tangu mwaka 2017 hadi sasa.

Anasema katika kipindi cha ‘Kenda Imani; anafahamika kwa majina tofauti ikiwamo mama Mbela pia dadake Ruth.

Kadhalika amewahi fanya kazi kwenye kituo cha Redio cha Ramogi FM kama mzalishaji wa vipindi pia alikuwa kati ya watayarishaji wa kipindi cha ‘Vyakula vyetu’ kilichokuwa kinapeperushwa kupitia KCB Televisheni.

Anadokeza kuwa hakuna sekta isiona changamoto. Anadai kuwa

ingawa visa vya ubaguzi wa rangi katika tasnia ya uigizaji vimepungua vimekuwa kati ya visingiti vinavyobomoa sekta ya maigizo hapa Kenya.

”Nyakati zingine hufanya kazi na maprodyuza husika kusepa bila kutulipa hali ambayo hufanya baadhi yetu kuvunjika moyo na kuwazia kuitema taaluma ya uigizaji. Aidha suala la malipo duni linazidi kutuponda bila kuweka katika kaburi sahau visa vya timu mafisi,” akasema.

Hata hivyo dada huyu siyo mchoyo wa mawaidha, anahimiza wanadada wenzie wafanye utafiti zaidi wajifunze masuala tofauti kuhusu maigizo hasa jinsi wanavyoweza kuibuka waigizaji bora.

You can share this post!

Wizara kuanzisha mpango wa kuufanya utoaji damu kuwa mazoea

Gravo Legends waingia KYSD, waapa kung’aa

adminleo