• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Gravo Legends waingia KYSD, waapa kung’aa

Gravo Legends waingia KYSD, waapa kung’aa

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gravo Legends inasadiki kuwa inatosha kutesa wapinzani wao kwenye kampeni za kinyang’anyiro cha kufukuzia ubingwa wa Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 14 muhula huu.

Ndio mwanzo kwa Gravo kushiriki kipute hicho lakini kocha wake, Zachariah Abdi anasema ameandaa wachezaji wake kutoa upinzani mkali dhidi ya wapinzani wengine wakiwamo mabingwa watetezi, Kinyago United.

”Ingawa ndiyo tunashiriki mechi za KYSD kwa mara ya kwanza kusema kweli wachezaji wangu wameonyesha wanaweza kufanya vizuri maana kwenye mchezo wetu na MASA uliozua msisimko wa aina yake walifaulu kusajili ushindi wa magoli 4-3,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa wakizoea kushiriki michuano yenye ushindani bila shaka watafanya vyema kwenye kampeni za misimu ijayo.

Kadhalika alidokeza kuwa kamwe hawataogopa wapinzani wengine kama Kinyago United, Sharp Boys na Volcano wanaozidi kutamba kwenye mechi hizo ambapo baada ya kushiriki patashika nane wamo katika nafasi tatu bora kwenye jedwali.

Kocha wa Gravo Legends, Zachariah Abdi akizungumza na wachezaji kabla ya kushuka dimbani kushiriki mojawapo wa mechi za Ligi ya KYSD. Picha/ John Kimwere

Kocha huyo amedai raundi hii anataka kuongoza vijana hao kuhakikisha wamefaulu kumaliza miongoni mwa nafasi tatu bora kisha kwenye mechi za msimu ujao watapigana kufa na kupona ili wahakikishe wametwaa ubingwa wa kipute hicho.

Kadhalika anakiri kuwa ngarambe hiyo imeonekana itashuhudia ushindani mkali kutoka kwa vikosi ambavyo siyo mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo. Nahodha wake, Hamza Abdirahman amesema “Baadhi ya timu zinazoshiriki ngarambe hiyo zimezoea upinzani uliopo baada ya kushiriki ndani ya misimu kadhaa iliyopita.”

Gravo Legends ilianzishwa mwaka 2010 ili kuleta vijana chipukizi katika mtaa wa Eastleigh pamoja kushiriki soka pia kuwasaidia kujiepusha dhidi ya kushiriki matendo maovu.

Kocha huyo anadokeza kuwa wameamua kushiriki migarazano ya msimu huu baada ya kutambua umuhimu wake kwa wachezaji chipukizi. ”Nimegundua kwamba mechi za ngarambe hiyo zimefanikiwa kukuza wachezaji wengi tu ambao wamesajiliwa kuchezea klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya KPL kama Gor Mahia FC kati ya zingine,” alisema.

Baadhi ya chipukizi wa MASA pia wanaoshiriki Ligi ya KYSD. Picha/ John Kimwere

Gravo Legends inshirikisha chipukizi kama: Vincent Bosire, Hamza Abdiragman (nahodha), Yussuf Mohamud, Khalid Mohammed, Adan Yussuf, Mohamed Abdullahi, Abdikadar Ahmed, Mohamed Amin, Salah Abdinur, Nadir Ali, Abdullahi Mohamud, Abdullahi Omar na Adnan Yussuf. Pia wapo Suheib Mohamed, Zakaria Abdinasir, Mahat Adan, Abdikadir Mohamed, Hamza Abdikarim, Omar Mohamed na Bashir Mohamed.

Jumla ya timu 16 zinashiriki kipute hicho cha muhula huu ambazo ni: Kinyago United, MASA, Sharp Boys, Young Elephant, Locomotive, Blue Boys, Young Achievers, State Rangers, Black Jack, Gravo Legends, Lehmans, Volcano, Fearless, Spartans, Fernabache na Ajax Pumwani.

You can share this post!

ANJELLA NANCIE: Walidhani nitakuwa mwanasayansi lakini...

Kinyago United wazidi kutesa KYSD

adminleo