Sh1000: Tuwakumbushe mama na nyanya zetu mashambani kuhusu noti mpya – CBK
Na CHARLES WASONGA
BENKI Kuu ya Kitaifa (CBK) imewataka Wakenya wawakumbushe mama na nyanya zao wanaoishi mashambani kuhusu kukaribia kwa tarehe ya mwisho ya kubadilishwa kwa noti za zamani za Sh1,000 na zile mpya.
Katika ujumbe iliyowekwa kwenye akaunti yake ya Twitter, CBK ilikariri kuwa baada ya tarehe hiyo, noti zote za zamani hazitatumika tena.
“Mama na nyanya zetu ni waweka akiba shupavu. Huenda wa kuhifadhi pesa zingine nyumbani. Tafadhali wafikie na mwakumbushe kuwa tarehe ya mwisho ya kubadilisha noti za zamani za Sh1,000 na zile mpya ingali Septembe 30. Endapo badi wanahifadhi noti za zamani tafadhali waambieni waziwasilishe kwa benki ili wapewe noti mpya,” CBK ikasema.
Inaaminika kuwa akina mama na nyanya katika jamii za Kiafrika hupenda kuhifadhi pesa katika nyumba zao. Hii ndio maana asasi hii ambayo husimamia sekta ya benki imetoa wito huu.
Kando na hayo, CBK imekuwa ikitoa wito huo kila siku kupitia matangazo yaliyolipiwa katika magazeti ya kila siku yanayochapishwa humu nchini, redio na runinga. Katika jumbe hizo umma hukumbushwa kuhusu siku ambazo zimesalia kabla ya muda wa matakataa uliowekwa kutamatika.
Kwa mfano, ujumbe wa Jumatano magazetini ulisoma hivi: “UKO TAYARI? ZIMEBAKI SIKU 20. Badilisha noti za elfu moja sasa! Usingoje dakika za mwisho!”
Ujumbe kama huo pia unapatikana katika wavuti ya CBK ambao ni www.centralbank.go.ke/deadline/.
Akiongea katika runinga moja ya humu nchini mapema mwezi huu Gavana wa Benki hii Patrick Njoroge alitoa wito kwa Wakenya kubadilisha noti zao za zamani kwa haraka kwani baada Septemba 30, noti hizo “zitageuka karatasi”.
Noti mpya za Sh1,000 zilianza kusambazwa kuanzia mwezi Juni mwaka huu baada ya kuzinduliwa rasmi wakati wa Sherehe za Kitaifa za Madaraka Dei zilizofanyika katika uwanja wa michezo wa Narok.
Dkt Njoroge alisema kuwa kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu zaidi ya noti 100 milioni kati ya noti 217 milioni za Sh1,000 zilikuwa zimereshwa katika CBK.