Afrika Kusini yazungumzia kushambuliwa kwa raia wa Nigeria
Na AFP na MARY WANGARI
AFISI ya Rais Nigeria imefichua ujumbe uliotumwa kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, na mjumbe maalum wa Rais Muhammadu Buhari, Bw Ahmed Rufai Abubakar, ambao umezingirwa na usiri.
Ujumbe wa Rais ulionyesha kwamba, serikali ya Afrika Kusini ilikanusha dhana ya jumla kuwa mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya raia wa kigeni nchini humo, ni ya ubaguzi wa rangi huku duru kutoka THISDAY zikisema maafisa wake wakuu walitaja idadi ya vifo tangu Desemba 2017 kuwa 89.
Abubakar, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Kitaifa ya Ujasusi (NIA), alitumwa Afrika Kusini wakati wa mashambulizi ya ubaguzi wa rangi yaliyotekelezwa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya Waafrika wenzao, ikiwemo raia wa Nigeria.
Mashambulizi hayo ambayo bado hayajakoma, yamefanya serikali ya Nigeria kuzidisha juhudi za kuwasafirisha raia wake wanaotaka kurejea nyumbani kutoka Afrika Kusini.
Kufikia sasa, raia 640 wa Nigeria wamejisajilisha kurejea nchini kwao.
Mipango ya usafirishaji inaendelea huku kukiwa na juhudi za kusuluhisha kwa njia ya amani tatizo hilo la kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili makuu Afrika.
Kulingana na mamlaka ya Afrika Kusini, kuna makundi matatu ya raia wa Nigeria nchini Afrika Kusini.
Kundi la kwanza ni wataalam wanaobobea katika nyanja za matibabu na elimu.
La pili ni wafanyabiashara, ikiwemo wauza bidhaa halali. La tatu ni wanaohusika na mihadarati.
“Hawa watu (walanguzi wa dawa za kulevya) ni wachache lakini wana sauti kubwa sana. Inasikitisha kuwa ndio wanaoonekana kama sura ya Nigeria nchini Afrika Kusini,” afisa mkuu mmoja alisema.
Licha ya dhana ya jumla, duru za THISDAY zilisema Jumanne kuwa Ramaphosa na maafisa wakuu wa serikali yake walisisitiza kuwa mashambulizi hayo yaliyosambaa si ya ubaguzi wa rangi.
Alifichua kuwa ingawa kati ya Desemba 2017 na Septemba 2019, raia 89 wa Nigeria waliuawa nchini humo, 39 miongoni mwao waliuawa na raia wenzao kutokana na migogoro inayohusu mihadarati.
Hata hivyo, Afrika Kusini ilikiri kuwa vifo 19 vilitokana na ukatili wa polisi huku vingine vikitokana na sababu nyinginezo.
Serikali ya Afrika Kusini pia ilisemekana kufichua kuwa kati ya raia 300,000 hadi 400,000 wa Nigeria wamo nchini Afrika Kusini.
Kwa sasa, 10,860 miongoni mwao wamo gerezani wakihudumu vifungo mbalimbali lakini asilimia 60 ya wafungwa wamo gerezani kutokana na uhalifu unaohusu mihadarati.