Makala

KIU YA UFANISI: Kwa mtaji wa kuku wa Sh10,000 hujipatia Sh20,000 kila mwezi

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER CHANGTOEK

ALIANZA kujishugulisha na kilimo cha ufugaji wa kuku takribani mwaka mmoja uliopita, na kwa sababu zaraa hiyo imenoga, ameamua kutotazama nyuma asilani.

Irene Chepkoech ni mkulima hodari wa kuku, na amekuwa akiendesha shughuli ya ufugaji wa kuku katika shamba lake lililoko katika kitongoji cha Kaptebeswet, kaunti ya Kericho.

“Nilianza kuwafuga kuku mnamo mwaka 2018, kwa kuutumia mtaji wa Sh10,000,’’ afichua mkulima huyo.

Chepkoech anasema kuwa yeye huwafuga kuku aina ya rainbow roosters ambao aliwanunua kutoka kwa kampuni moja katika kaunti ya Uasin Gishu.

“Nilianza kwa kuwafuga vifaranga mia moja ambao niliwanunua kutoka kwa kampuni ya Kukuchic iliyoko mjini Eldoret,’’ adokeza mkulima huyo, ambaye ni mama wa watoto watatu.

Huvitumia vibanda viwili ambavyo vina urefu wa futi kumi na mbili na upana wa futi kumi.

Aidha, huwafuga ndege hao kwa kulitumia shamba la nusu ekari, ambapo kuku huruhusiwa kutembeatembea shambani.

Mbali na kuruhusiwa kutembeatembea shambani kuzitafuta lishe, kuku wa mkulima huyo hupewa lishe aina ya ‘growers mash’, mboga aina tofauti tofauti, nyasi aina ya mabingobingo (Napier grass) pamoja na lishe nyinginezo nyingi.

Chepkoech anadokeza kwamba kuku wake hupewa lishe hizo mara mbili kwa siku. Yeye huzinunua lishe hizo kutoka kwa duka la kuuza bidhaa za kilimo na lishe za mfugo, lijulikanalo kwa jina Tulwet Agrovets, lililoko mjini Kericho.

Mkulima huyo anafichua kuwa idadi kubwa ya kuku ambao amewahi kuwa nao ni kati ya mia tatu na mia nne, na yeye huwauza ndege hao kila mara.

Chepkoech anaongeza kwamba yeye huwauza kuku wake wakiwa wadogo, kabla hawajakomaa na kuanza kuyataga mayai.

Mkulima huyo anasema kuwa yeye ana mikakati bora inayomwezesha kuwahudumia kuku wake na kuhudumu kazini pasi na kuhujuma upande wowote, kwa kuzingatia ratiba yake kikamilifu.

Mkulima huyo huwauza kuku wake kwa bei tofauti tofauti, kuambatana na umri ambao ndege hao wanao. Yeye huwauza vifaranga wenye umri wa mwezi mmoja na wiki tatu kwa bei ya Sh350, ilhali wale wenye umri wa miezi miwili hadi mitatu huuzwa kwa Sh500.

Mitandao

Chepkoech, aghalabu, huwauza kuku wake kupitia kwa mitandao ya kijamii, ambapo hutagusana na wateja, na hatimaye kuwauzia wale walio na nia ya kuwanunua.

“Huwauza kwa WhatsApp, Facebook, na kwa vikundi mbalimbali vya wakulima vilivyomo mitandaoni,’’ aongeza mkulima huyo.

Hakuna jambo lisilokuwa na changamoto. Licha ya mkulima huyo kuwa na ufanisi katika shughuli hiyo, anafichua kwamba kuna baadhi ya changamoto ambazo amekumbana nazo.

 

Bi Irene Chepkoech akionyesha baadhi ya kuku anaowafuga katika eneo la Kaptebeswet, kaunti ya Kericho. Picha/ Peter Changtoek

Mojawapo ni mwewe ambao huwavamia kuku wake na kuwala. Fauka ya hayo, kuna changamoto ya kuwapata wateja wa kuwauzia kuku wake.

Mbolea za kuku ambazo mkulima huyo hukusanya kutoka kwa ndege wake, huzitumia kuipanda mimea kama vile mboga, migomba, maua, miongoni mwa mimea mingineyo.

Mkulima huyo anafichua kuwa biashara hiyo ina tija, na yeye hutia kibindoni hadi Sh20,000 kwa mwezi biashara inapokuwa bora.

Mbali na ufugaji wa kuku, yeye pia, hujishughulisha na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na ana biashara mjini Kericho.

Anawashauri wale wanaopania kujitosa katika shughuli ya ufugaji wa kuku kufanya hivyo, maadamu “huhitaji mtaji mdogo.’’ Aidha, anaongeza kuwa shughuli hiyo ni rahisi kuitekeleza.

Aidha, anafichua kuwa mipango yake ya siku za usoni ni kukiendeleza kilimo hicho kwa kuongeza idadi ya kuku anaowafuga.