Habari

MAU: Wabunge wataka Tobiko awaandame 'samaki wakubwa'

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu kutoka Rift Valley sasa wako tayari kuunga mkono mpango wa serikali wa kuwaondoa watu walionyakua ardhi kinyume cha sheria katika msitu wa Mau ikiwa serikali itasambaza operesheni hiyo katika maeneo yaliyokaliwa na matajiri.

Wabunge hao; Hillary Kosgei (Kipkelion Magharibi), Beatrice Kones (Bomet) na Charity Kathambi Chepkwony (Njoro) Jumatano walimwambia Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko kwamba wataamini kuwa serikali haiwaonei watu wadogo ikiwa itawaandama “samaki wakubwa”.

“Tunataka waziri Tobiko afahamu kwamba hatupingi mpango wa serikali wa kuhifadhi msitu wa Mau. Kile tunapinga ni kuendeshwa kwa shughuli kwa njia ya ubaguzi ambapo watu maskini ndio wanalengwa ilhali matajiri ambao pia walinyakua ardhi katika msitu huo wanasazwa,” akasema Bw Kosgei.

Naye Bi Chepkwony akauliza: “Tunawafahamu matajiri wengi wanaomiliki ardhi katika msitu wa Mau kinyume cha sheria ambako wanakuza majani chai, lakini mbona ni watu maskini ndio wanafurushwa kutoka eneo la Maasai Mau?”

“Tunataka Bw Tobiko aanze pia kuondoa matajiri walionyakua Msitu wa Mau katika maeneo kama vile Kiptagich. Akifanya hivyo, tutaunga mkono mchakato huu kwa moyo wetu wote,” akaongeza Mbunge huyo wa Njoro.

Jamii moja

Kwa upande wake Bi Kones, alimsuta waziri Tobiko kwa kulenga watu kutoka jamii moja pekee katika awamu wa pia ufurushaji watu kutoka msitu wa Mau, akishauri kuwa shughuli hiyo haifai kuingizwa ukabila.

Wabunge hao walikuwa wakiongea bungeni Jumatano siku moja baada ya Tobiko kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira ambapo alitoa hakikisho kuwa serikali itawaandama watu wengine walionyakuwa ardhi ya misitu; sio tu katika Mau bali misitu mingineyo nchini.

“Natoa onyo kwa wengine wote kwamba hawatasazwa. Baaada ya kukamilisha awamu ya pili ya ufurushaji watu kutoka eneo la Maasai Mau tutawaandama wale wengine walionyakuwa ardhi katika Mau kinyume cha sheria,” Bw Tobiko akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Maara, Kareke Mbiuki.

Waziri alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kutoa ufafanuzi kuhusu mantiki ya shughuli inayoendelea sasa ya kufurusha familia 16,000 zinazoishi katika eneo la Msitu wa Maasai Mau.

Bw Tobiko aliwaomba wanachama wa Kamati hiyo wamuunge mkono kwa njia zozote zile wakati ambapo ataanza kuwaandama “samaki wakubwa” katika Mau na misitu mingine kama Aberdares na Mlima Kenya.

Rais Mstaafu Moi ni baadhi ya watu mashuhuri wanaodaiwa kumiliki vipande vikubwa vya ardhi katika msitu wa Mau.

Mzee Moi anamiliki Kiwanda cha Majani Chai cha Kiptagich kilichoko katika ardhi ya ukubwa wa ekari 2,223, 945.