HEDHI: Millie Odhiambo aghasika baada ya mwanafunzi kujitia kitanzi kwa kudhalilishwa
Na SARAH NANJALA na MARY WANGARI
WIZARA ya Elimu imeangaziwa kufuatia kifo cha mwanafunzi wa darasa la sita aliyejitia kitanzi baada ya kuaibishwa na mwalimu kwa sababu ya hedhi huku Mbunge wa Suba Kaskazini, Millie Odhiambo, akiitaka familia iliyoathiriwa kuishtaki wizara kwa kumpoteza mtoto wao.
Akizungumza na Taifa Leo katika mahojiano kwa njia ya simu, mnamo Alhamisi, mbunge huyo pia amesema kifo cha msichana huyo wa umri mdogo kilikuwa matokeo ya Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) kukosa kuwapa mafunzo walimu wao na kutoa sodo ambazo tayari zimepangiwa katika bajeti.
“Sodo za wasichana tayari zimejumuishwa katika bajeti. Hivi ni vitu ambavyo huwezi kuchelewesha katika wizara kwa sababu kinyume na miundomsingi, hedhi haiwezi kungoja,” amesema Odhiambo.
Aidha, Odhiambo amesema hatua za kinidhamu zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya mwalimu aliyesababisha kadhia hiyo kutokea akisema kuwa, kisa hicho ni ishara bayana ya kiwango cha kukosa ufahamu miongoni mwa walimu kuhusu kukabiliana na masuala kama vile hedhi.
“Pana haja ya uhamasishaji kuhusu masuala ya uzazi kwa sababu hedhi ni jambo la kawaida na wasichana wanapaswa kufahamishwa hayo. Kwa mwalimu husika, kitendo cha kuaibisha si kitu kikubwa lakini kwa mwanafunzi ni jambo la kuaibisha mno,” alisema.
Isitoshe, muunda sheria huyo alisema Wizara ya Elimu ina malighafi nyingi ya elimu kuhusu uzazi inayoweza kutumiwa shuleni na kuongezwa katika mtaala.
Kisa cha Jackline Chepngeno mwenye umri wa miaka 14 kiligonga vyombo vya habari na kuibua ghadhabu nchini na kimataifa baada ya kupatikana akining’nia kwenye mti karibu na boma lao, muda mfupi baada ya kuondoka shuleni, ambapo mwalimu wake wa Kiingereza alimdhihaki na kumdhalilisha kwa kukosa sodo.
Wanawake kutoka eneo jirani walifurika shuleni humo wakitaka kujua ni kwa nini mwalimu huyo alimfedhehesha msichana huyo.