RONALDO MUUAJI! Ureno yaipiga Lithuania 5-1
Na MASHIRIKA
VILNIUS, Lithuania
MSHAMBULIAJI matata Cristiano Ronaldo alipachika wavuni mabao manne na kuisaidia Ureno kuibuka na ushindi wa 5-1 Jumanne usiku dhidi ya Lithuania katika pambano la kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Euro 2020.
Staa huyo wa klabu ya Juventus ambaye amefikisha mabao 93 ya kimataifa alifunga bao la mapema kupitia kwa mkwaju wa penalti kabla ya Vytautas Andriukevicius kusawazisha.
Ronaldo alifunga bao la pili kutokana na kombora la umbali wa yadi 20 ambalo lilimchanganya kipa Ernestas Setkus, kabla ya kufunga mengine mawili kutokana na pasi ya Bernardo Silva. Bao la tano lilifungwa na William Carvalho katika muda wa majeruhi.
Ushindi huo umeihakikishia Ureno nafasi ya kufuzu kwa Euro 2020, wakiwa pointi tano nyuma ya vinara Ukraine katika KUNDI B.
Hii ilikuwa mara ya nane kwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 kufunga mabao matatu katika mechi moja ya kimataifa. Aliwahi kufunga matatu dhidi ya Abdorria mnamo 2016.
Serbia wamesonga hadi nafasi ya tatu baada ya kuandikisha ushindi wa 3-1 dhidi ya Luxembourg, katika mechi ambayo Aleksandar Mitrovic alifunga mawili.
Kwingineko, Antoine Griezmann alipoteza penalti ya pili ndani ya siku nne, lakini kikosi chake cha Ufaransa kikaibuka na ushindi dhidi ya Anndorra katika pambano la mchujo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwa Euro 2020.
Kingsley Coman alimzungusha kipa Josep Gomes kabla ya kuwapa washindi bao la kwanza, lakini kipa huyo alifanya juhudi na kunyaka penalti ya Griezmann.
Pasi
Hata hivyo, Griezmann alimuandalia pasi mwenzake wa Barcelona, Clement Lenglet pasi kufungia Ufaransa bao la pili.
Wissam Ben aliongeza la tatu baada ya frikiki ya Nabil Fekir kumchanganya kipa Gomes. Hii ilikuwa penalti ya tatu kwa Griezmann kupoteza baada ya kupoteza nyingine katika ushindi wao wa 4-1 mnamo Jumamosi.
Andorra imeshindwa mechi zote 56 za mchujo wa kufuzu tangu waanze kushiriki katika michuano hiyo ya bara Ulaya. Licha ya ushindi huo, Ufaransa wameshuka hadi nafasi ya pili katika Kundi H, baada ya vinara Uturuki kuibuka na uahindi wa 4-0 dhidi ya Moldova.
Iceland inafuatia baada ya kuibuka na ushindi wa 4-2 dhidi ya Albania, ambao wako nyuma kwa tofauti ya pointi sita kwenye kundi ambalo timu mbili za kwanza zitafuzu kwa namna ya moja kwa moja.
Matokeo ya mechi za mwishoni mwa wiki kwa ufupi: Estonia 0 Uholanzi 4; Iceland Kaskazini 0 Ujerumani 2; Azerbaijan 1 Croatia 1; Hungary 1 Slovakia 2; Latvia 0 Macedonia 2; Poland 0 Austria 0, Slovania 3 Isreal 2; Armenia 4 Bosania-Hezegovina 2; Finland 1 Italia 2; Ugiriki 1 Liechtenstein 1; Georgia 0 Denmark 0; Uswizi 4 Gilbraltar 0; Romania 1 Malta 0; Uhispania 4 Visiwa vya Faroe 0; Sweden 1 Norway 1.