Tutapigana kufa kupona, kocha wa Malkia Strikers aahidi
Na JOHN KIMWERE
KOCHA mkuu wa timu ya voliboli ya wanawake maarufu Malkia Strikers, Paul Bitok amesema kuwa analenga kuhakikisha kikosi hicho kinafaulu kushinda mechi mbili ama tatu kwenye kipute cha Kombe la Dunia kitakachoanza mwezi huu, Septemba 14 -19 nchini Japan.
Kocha huyo amefunguka kwamba kampeni za mashindano hayo zitakuwa ngumu hasa kwa wawakilishi wa bara Afrika Kenya na Cameroon.
“Binafsi kama kocha wa Malkia Strikers nimepania kuwapa wachezaji chipukizi nafasi kushiriki mashindano ya hadhi ya juu kwenye jitihada za kuunda kikosi imara siku zijazo,” alisema na kuongeza tayari ameongea na shirikisho kuhusu suala la kuwa na timu tatu za taifa.
Malkia Strikers ilitarajiwa kuondoka baadaye jana kuelekea nchini Japan tayari kushiriki kinyang’anyiro hicho.
Kenya na Cameroon zitashiriki ngarambe hiyo baada ya kumaliza kati ya nafasi mbili za kwanza kwenye mashindano ya Michezo ya Afrika (AAG) iliyofanyika Agosti jijini Rabat, Morocco.
Kwenye fainali ya pambano hilo, Malkia Strikers ilikomoa Cameroon seti 3-1 na kuhifadhi taji hilo ililotwaa kwenye makala ya mwisho yaliyofanyika jijini Brazzaville, nchini Congo mwaka 2015.
Kwenye ratiba ya ngarambe hiyo Malkia Strikers itafungua kampeni zake dhidi ya Marekani Jumapili mjini Hamamatsu. Mjini Hamamatsu, Kenya ilitacheza na Argentina, Brazil, Serbia, Uholanzi na Marekani.