Serikali yapiga marufuku raia wa kigeni kuchukua na kulea watoto wa humu nchini
Na MARY WANGARI
RAIS Uhuru Kenyatta amepiga marufuku mara moja raia wa kigeni kuchukua na kuwalea watoto wa nchini Kenya huku akiagiza Wizara ya Leba kuunda sera mpya ya kudhibiti upangaji watoto na raia wasio Wakenya.
Hatua hiyo ilitangazwa jana katika mkutano maalum wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Ikulu, Nairobi, na ulioongozwa na Rais akiwa ni mwenyekiti wake na kuhudhuriwa na Naibu Rais William Ruto.
Kiongozi wa Taifa pia ameagiza Wizara ya Leba na Ulinzi wa Jamii kubuni sera mpya za kudhibiti shughuli ya upangaji wa watoto na raia wa kigeni nchini Kenya.
Aidha, Wizara hiyo imeagizwa kulainisha shughuli za Shirika la Maslahi ya Watoto Kenya pamoja na shughuli za makao ya watoto nchini.
Baraza hilo pia liliidhinisha Sh6.9 bilioni kwa lengo la kuendeleza miundomsingi katika eneo maalum lililotengwa Naivasha pamoja na ukamilishaji wa awamu ya pili ya Standard Gauge Railway (SGR).
Katika baraza hilo vilevile, uidhinishaji wa kuandaliwa kwa warsha ijayo Nairobi ya Kongamano la Kimataifa kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo awamu ya 25 (ICPD), ulipitishwa.
Kongamano hilo lililopangiwa kufanyika kuanzia Novemba 12 hadi 14, 2019, linatarajiwa kuvutia wajumbe zaidi ya watu 6,000 kutoka mataifa 179.
Warsha hiyo inatazamiwa kupiga jeki sekta ya utalii nchini Kenya kwa kutoa picha nzuri na kuimarisha nafasi ya Kenya kama kituo mwafaka cha kongamano na usafiri wa ndege.