Ruto mawindoni Pwani siku tano
MOHAMED AHMED na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais William Ruto jana alianza rasmi ziara ya siku tano eneo la Pwani baada ya kukaa kwa miezi miwili bila kuzuru eneo hilo.
Ziara yake hiyo ilijiri siku tatu pekee baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru eneo hilo na kukagua miradi ya maendeleo.
Tofauti na awali alipokuwa akiandamana na Rais katika shughuli za kiserikali na kijamii, Dkt Ruto amekuwa akiepuka hafla hizo na kuandaa zake binafsi na wanasiasa wanaomuunga mkono.
Wandani wake eneo hilo kama vile mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Msambweni Suleiman Dori wamekuwa kimya kwa muda ambao hajatembelea Pwani.
Dkt Ruto alitembelea eneo la Bura kaunti ya Tana River ambapo alikagua sehemu ya kwanza ya mradi wa kunyunyuzia maji mashamba wa Bura utakaogharimu Sh1.7 bilioni na kusisitiza msimamo wa serikali kuhusiana na ajenda zake nne ambazo zinahusisha kuhakikisha uwepo wa chakula cha kutosha nchini.
Bw Ruto alisema kuwa serikali ina azma ya kupambana na baa la njaa na kuona wananchi wanapata chakula cha kutosha. Vile vile, alipeana mbegu za korosho na nazi kwa wakazi wa eneo hilo.
Leo, kulingana na ratiba kutoka kwa wasimamizi wake, atakuwa katika kaunti ya Kilifi ambapo anatarajiwa kukagua daraja la Shakahola na baadaye kufungua mradi wa maji wa Baricho.
Siku ya Jumamosi, Dkt Ruto anatarajiwa kaunti ya Mombasa kwa ajili ya ufunguzi wa mitaro ya maji eneo la Changamwe kabla ya kuelekea kaunti ya Kwale ambapo anatarajiwa kufungua mradi wa bwawa la Pemba lililojengwa kwa gharama ya Sh500 milioni.
Mnamo Jumatatu, Dkt Ruto atahitimisha ziara yake ya siku tano kwa kuelekea kaunti ya Taita Taveta ambapo atakagua mradi wa kunyunyiza maji mashamba wa Njoro Kubwa.
Wakati wa ziara yake wiki jana, Rais Kenyatta pia alizuru maeneo ya kaunti za Lamu, Mombasa na Kwale ambapo alikagua baadhi ya miradi.
Katika ziara hiyo, Rais Kenyatta hakuwa ameandamana na Bw Ruto ambaye mara mwisho kuwa Pwani ilikuwa ni mwezi Juni ambapo alihudhuria harambee ya kuchangia kutafsiriwa kwa Bibilia kwa lugha ya Giriama eneo la Kilifi.
Wakati huo, ilikuwa ni ziara yake ya tisa eneo la Pwani tangu muafaka wa Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9.
Hapo awali, Dkt Ruto alikuwa akizuru Pwani mara kwa mara na kumpelekea kupigwa jeki katika azima yake ya kugombea urais baada ya wabunge kadha wa eneo hilo kutangaza kuwa watamuunga kwenye uchaguzi wa 2022.
Aidha, wapinzani wa Bw Ruto pia walianza kutoa cheche za kisiasa na kumshtumu kwa kuanza kampeni za mapema kwa sababu ya ziara zake za eneo la Pwani na maeneo mengine ya nchi.
Dkt Ruto alilazimika kuzungumzia suala hilo na kusema kuwa ziara zake hizo zilikuwa zinalenga maendeleo tu japo wandani wake wamekuwa wakizungumzia siasa.
Baada ya hapo alipunguza ziara hizo na kupelekea eneo la Pwani kutulia kisiasa hadi sasa.