Mbunge aandaa mswada wa kuhakikisha hospitali zinaweka mikakati salama ya kushughulikia takataka
Na CHARLES WASONGA
MBUNGE wa Kesses, Swarup Mishra ameandaa mswada unaolenga kulazimisha hospitali za umma na zile za binafsi kujenga miundomsingi ya kuondoa taka kwa njia salama.
Mbunge huyo alisema Alhamisi hospitali nyingi nchini huwa hazina mifumo mizuri ya kushughulikia takataka; hali ambayo huwa hatari kwa afya ya umma.
Mswada huo unalenga kuweka kanuni madhubuti ya kushughulika takataka zinazotokana na shughuli za upasuaji kama vipande vya mwili wa mwanadamu, vifaa vya matibabu ambavyo hupata alama za damu kama shindano, visu na glavu.
Dkt Mishra ambaye ni mtaalamu wa upasuaji anasema kuwa kutoshughulikiwa vizuri kwa takataka kutoka hospitali na vituo vya kiafya huchangia asilimia 50 ya magonjwa ya kuambukiza humu nchini.
“Ikiwa mswada huu utapitishwa na kuwa sheria hatari ya kuenea kwa maradhi ya kuambukiza na yale yanayowaathiri wafanyakazi mahala pa kazi yatapungua,” akasema Dkt Mishra ambaye ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Afya, katika majengo ya bunge Jumatano jioni.
Wakati huu, takataka nyingi kutoka vituo vya afya huishia katika majaa mbalimbali katika miji mikuu.
Hali hii huwaweka hatarini watu ambao huchakura takataka hizo kutafuta vitu vya thamani kama plastiki na hata chakula.