Mahakama yaagiza shule zisiwe zikifukuza wanafunzi wenye nywele za rasta

Na MARY WANGARI

MAHAKAMA KUU imeagiza shule zisiwe zikiwafukuza wanafunzi wenye nywele za rasta huku jaji akisema Rastafari ni imani ya kidini inayotambulika.

Ni uamuzi muhimu uliotolewa na Mahakama Kuu jijini Nairobi kuhusiana na kesi ambapo shule ya umma ilikataa kumsajili mwanafunzi kwa kukataa kunyoa nywele zake aina ya rasta.

Umeibua hisia mbalimbali miongoni mwa watumiaji mitandao ya kijamii.

Jaji wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita, mnamo Ijumaa, Septema 13, 2019, katika uamuzi wake alisema hatua ya shule hiyo ilikuwa kinyume na Katiba maana nywele hizo za Makeda Ndinda ziliashiria imani yake.

Isitoshe, Jaji Mwita alisisitiza kuwa Rastafari ilikuwa dini kama nyingine yoyote ile.

“Mtoto ana haki kikatiba ya elimu ya kimsingi. Kuweka rasta (dreadlocks) ni njia ya kukiri imani yake na ni hatia kumshurutisha anyoe hatua ambayo ni kinyume na dini yake,” alisema jaji huyo.

Uamuzi huo umejiri kufuatia kesi iliyowasilisha na babake mtoto huyo, John Mwendwa dhidi ya shule ya upili ya Olympic katika eneobunge la Kibra, akilalamikia dhidi ya hatua ya shule hiyo ya kukataa kumsajili bintiye, huku akiitaja kama ubaguzi dhidi ya mtoto wake pamoja na imani yake ya Rastafari.

Januari 2019 Jaji Mwita alikuwa ametoa amri ya kumruhusu Ndinda kusajiliwa shuleni huku uamuzi wa kesi hiyo ukisubiriwa.

Kufuatia uamuzi huo Wakenya walijitosa mitandaoni huku jaji huyo akipokea kiwango sawa cha pongezi na shutuma.

Wafuasi wa Rastafari walijawa na furaha huku baadhi wakosoaji wao wakishindwa kuzuia hisia zao wakihoji kwamba uamuzi huo utatoa nafasi kwa makundi mengine kudai kutambuliwa vilevile.

“Ni tumaini langu sasa kwamba wasichana Waislamu wataruhusiwa uhuru sawia wa kuashiria dini yao shuleni,” alisema Kigen Koech

“Jaji huyu ni lazima awe mfuasi wa rastafarianism. Upuzi kama huo, ukosefu wa ujuzi, upumbavu na kukosa maarifa ya sheria,” akasema J Owaga.

“Uhuru wa dini umeangaziwa katika katiba. Pongezi kwa mheshimiwa jaji na mahakama,” alisema Sammie.

Kwa wengine, uamuzi huo uliwapa fursa murwa ya kupigia debe uhalalishaji wa bangi suala ambalo limekabiliwa na utata katika siku za hivi karibuni.

“Na ulijua sakramenti takatifu ya Rastafari ni Ganja almaarufu Tire! Uamuzi huu umetoa msingi mzuri mno kwa uhalalishaji wa marijuana,” alihoji Steve Ochie

Habari zinazohusiana na hii

Leave a Reply