Mashabiki wa Real kumuona Hazard leo Jumamosi
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
Kocha Zinedine Zidane alisema Ijumaa kuwa sajili mpya Eden Hazard amepata idhini ya kusakatia Real Madrid kwenye Ligi Kuu ya Uhispania kwa mara ya kwanza itakapokutana na Levante, leo Jumamosi.
“Sote tunatamani kumuona Eden,” alianza Zidane.
“Kuna presha sana kwake na pia matarajio ni makubwa. Hata hivyo, yuko sawa na hicho ndicho kitu muhimu.”
Hazard alitarajiwa kusakata mechi yake ya kwanza dhidi ya Celta Vigo katika raundi ya ufunguzi mnamo Agosti 17 baada ya kutua uwanjani Santiago Bernabeu kutokea Chelsea kwa Sh11.5 bilioni mwezi Juni.
Hata hivyo, Mbelgiji huyo alipata jeraha la paja katika uwanja wa mazoezi wa Real, Valdebebas, na kukaa mkekani wiki tatu katika kipindi ambacho klabu hiyo mpya kwake ilichechemea uwanjani, ikiambulia ushindi mmoja na sare mbili.
Zidane, hata hivyo, aliwataka mashabiki wawe na subira Hazard akipona.
“Lazima tuende taratibu,” alisema. “Hazard alikuwa na jeraha wiki tatu, amerejea mazoezini wiki moja.
“Tutasakata mechi saba ndani ya siku 21 na tutalazimika kumuonjesha mechi polepole. Itakuwa jukumu langu kuamua namchezesha dakika ngapi nikimtazama kwa sababu tunamhitaji kwa muda mrefu, kwa mechi nyingi, si mechi moja tu.”
Habari nzuri
Kurejea kwa Hazard ni habari nzuri kwa Madrid ambayo itaanza kampeni yake ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain juma lijalo, hasa kwa sababu Luka Modric aliingia mkekani baada ya kuumia kinena juma hili.
“Msimu unaanza sasa,” alisema Zidane. “Tuna orodha ya mechi saba katika siku 21 na nadhani hicho ndicho tunahitaji; kucheza, kuwa na uwezo wa kuamua mwelekeo wa mechi, kushindana… hivyo ni vitu wachezaji wanataka.”
Mfaransa Zidane pia alipuuzilia mbali wanaokosoa timu baada ya kutapa mwanzo wa msimu.
“Matamshi hayo, kila kitu kinachosemwa, mambo hayatabadilika,” alisema.
“Tunajua kile tunachotaka katika timu, tutajitahidi vilivyo kuhakikisha tunafanya vitu inavyopaswa. Maneno yametosha, lazima tuonyeshe matokeo uwanjani.”