Habari Mseto

Kenya kuandaa warsha ya kwanza ya ukufunzi barani Afrika

September 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANDISHI WETU

KENYA itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa warsha ya kwanza kuhusu mafunzo ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali wiki ijayo.

Katika warsha hiyo, Bi Emily Kamunde (pichani juu) kutoka Kenya ambaye ndiye Mwafrika kwa kwanza kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa bodi ya kimataifa ya Muungano wa Kimataifa kuhusu Mafunzo (ICF) ataungana na wakurugenzi wengine kuhutubu kuhusu umuhimu wa mafunzo ya viwandani.

Awali, Bi Kamunde alikuwa rais wa ICF – muungano wa hapa nchini, kando na kuwa mkufunzi wa mashirika na wafanyakazi kuhusu mbinu za kuimarisha utendakazi, kwa miaka kadhaa.

Warsha hiyo itakayofanyika kati ya Septemba 19 na 21 itakuwa ikilenga kueneza umuhimu wa kuwaongezea wafanyakazi maarifa katika bara la Afrika.

“Kabla ya mkuitano huo, bodi ya kimataifa ya ICF itaandaa jukwaa la mtagusano kwa wakufunzi wa Kenya na wataalamu wa nguvu kazi.

“Wakati wa warsha hiyo, wakurugenzi wa ICF pamoja na Bi Kamunde, wataelezea mipango ya kuongeza usemi wa ICF barani Afrika ili kuwafaidi wafanyakazi na mashirika,” ikasoma taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Maafisa wa nguvu kazi watakaohudhuria mkutano huo watajifunza mengi kuhusu maana ya ukufunzi wa viwandani, na jinsi wanaweza kuboresha kiwango cha utendakazi miongoni mwa wafanyakazi.

Ukufunzi wa viwandani ni mojawapo ya taaluma zinazokua zaidi ulimwenguni, huku utafiti wa

PricewaterhouseCoopers ukionyesha kuwa taaluma hiyo inazidi kusambaa duniani na kuunda nafasi nyingi za ajira.

Ni taaluma ambayo haibagui sekta yoyote na huongezea ubora wa kila pembe ya maisha, iwe familia, afya, biashara, teknolojia, uanasheria, ualimu, udaktari, uanahabari, uanasiasa, uanaspoti miongoni mwa taaluma nyinginezo.