• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 5:55 AM
FUNGUKA: ‘Twachuna ngozi moja…’

FUNGUKA: ‘Twachuna ngozi moja…’

Na PAULINE ONGAJI

KUBA tafiti kadha zinazosema kwamba pacha wanapozaliwa, wao huwa na uhusiano wa kipekee hasa kutokana na muunganisho waliokuwa nao tokea wawe tumboni.

Kumekuwa na hadithi hata za baadhi yao kuwa na uhusiano wa karibu sana kiasi cha kutokubali kutenganishwa mmoja wao anapooa au kuolewa.

Ni hali inaowakumba Jackson na Jeremy, pacha na wakazi wa sehemu ya Nakuru. Wawili hawa walizaliwa miaka 35 iliyopita na tangu watue hapa duniani, yaonekana kana kwamba kukatwa kwa mji wa mtoto (placenta), hakukuwatenganisha kamwe.

“Uhusiano wetu ni wa kipekee. Sote tulisoma pamoja katika darasa moja tokea shule ya chekechea hadi chuo kikuu. Hata tulipojiunga na shule ya upili ya mabweni, tulilala kwenye bweni na kijichumba kimoja.

Pamoja tumesomea taaluma ya udaktari na tunafanya kazi katika hospitali moja. Tumewekeza ambapo kwa pamoja tunamiliki mali kadha ikiwa ni pamoja na jumba moja la kifahari mjini Nakuru, magari kadha, na biashara mbalimbali.

Tunaishi katika nyumba moja na pia tunalala katika chumba kimoja. Isitoshe, tokea utotoni tumekuwa tukivalia mavazi yanayofanana kutoka utosini hadi mguuni.

Mtindo wa kunyoa ni ule ule ambapo tumesisitiza kwamba endapo mmoja atamtangulia mwenzake mautini, basi atakayesalia hatokuwa na budi ila kujitoa uhai kwani haiwezekani kwa mmoja wetu kuendelea kuishi bila mwenzake.

Hata katika masuala ya mapenzi, habari ni ile ile. Sote tumemuoa binti mmoja; mwanamke ambaye tunampenda sana.

Tumekuwa katika uhusiano huu kwa miaka kumi sasa na hata tumejaliwa watoto wanne. Maisha yetu ni ya kawaida kiasi kuwa kama wanandoa wengine, mke wetu ana majukumu ya upishi, uzazi na usafi nyumbani, huku sisi waume tukiwajibikia mahitaji yote ya kifedha.

Mke wetu hafanyi kazi kwani tuna pesa za kutosha, na badala yake jukumu lake kuu ni la malezi.

Sote tunachukulia watoto hawa kuwa wetu na sote tuna jukumu la kukidhi mahitaji ya kila mmoja, vilevile kuwaadhibu pasipo upendeleo.

Tunalala katika chumba kimoja na katika masuala ya mahaba lazima kila mmoja ashiriki. Mke wetu hulala katikati na kila mmoja hupata fursa ya kuhisi joto lake. Pia wakati wa mahaba, hali ni ile ile; kila mmoja ana zamu yake. Ikiwa mmoja ni mgonjwa, waliosalia hawana budi ila kumsubiri kupata nafuu.

Kwa kawaida sisi hushauriana kuhusu masuala yote katika nyumba yetu ikiwa ni pamoja na fanicha, chakula cha kupika, shule ambayo watoto watasomea na hata mahali pa kwenda likizoni au hata kuishi.

Wikendi inapofika, huandamana deti pamoja. Mke wetu anaposhika mimba na kukaribia kujifungua, sharti sote tuchukue likizo na kumsaidia.

Hatuna muda wa wivu katika uhusiano wetu na wazazi huwa tayari kutushauri tunapokumbwa na misukosuko kwani hata wao wamekumbatia uhusiano huu.

Uhusiano wetu ni wa kipekee na tunawashauri mapacha wengine wasiotaka kutenganishwa eti kwa sababu ya ndoa kukumbatia hilo”.

You can share this post!

Vikao vya Seneti kufanyika Kitui wiki ijayo

Nzoia Sugar FC yasalia bila ushindi kwenye Ligi Kuu

adminleo