Habari Mseto

Mariga kujua hatima yake Jumatatu

September 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na COLLINS OMULO

MWANIAJI wa chama cha Jubilee kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra, McDonald Mariga, atajua iwapo atagombea kiti hicho Jumatatu ambapo uamuzi wa rufaa aliyokata utatolewa.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati alisema Ijumaa kuwa kamati maalum inayosikiliza kesi iliyowasilishwa na mwanasoka huyo itatoa uamuzi wake siku hiyo.

Hii ni baada ya pande zote zinazohusika kwenye kesi hiyo kumaliza kuwasilisha maelezo yake Ijumaa.

IEBC ilimuondoa Mariga miongoni mwa wanaowania wadhifa huo Jumanne wiki iliyopita, baada ya jina lake kukosekana kwenye sajili kuu ya wapigakura.

Kutokana na hilo, tume hiyo ilisema kuwa hawezi kushiriki kwenye uchaguzi huo wa Novemba 7.

Kulingana na sheria za tume hiyo, lazima mwaniaji yeyote awe amesajiliwa kama mpigakura.

“Kwa kuwa pande zote husika zimemaliza kuwasilisha maelezo yake, tutatoa uamuzi wetu Jumatatu saa nne asubuhi,” akasema Bw Chebukati.

Mwenyekiti huyo alikuwa ameandamana na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu, ambao walikuwa kati ya washiriki wa kamati iliyokuwa ikisikiliza rufaa hiyo.

Mawakili wa Mariga

Wakitoa maelezo yao mbele ya kamati hiyo, mawakili wa Bw Mariga wakiongozwa na Elisha Ongoya waliomba kamati hiyo kumruhusu mlalamishi kushiriki kwenye uchaguzi huo.

Bw Ongoya alisema kuwa msimamizi wa uchaguzi katika eneobunge hilo, Bi Beatrice Muli, ambaye ndiye mshtakiwa alikosea kumzuia Bw Mariga kuwania wadhifa uo.

Alisema kuwa hatua hiyo itamnyima haki Bw Mariga na kuwanyima wapiga kura nafasi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Simlaumu msimamizi wa uchaguzi kwa kufanya kosa hilo. Hata ikiwa ni kosa alilofanya kimakusudi, linapaswa kurekebishwa na tume ili kuwapa nafasi wakazi wa Kibra nafasi ya kumchagua kiongozi wamtakaye,” akasema.

Hata hivyo, upande unaopinga Bw Mariga kujumuishwa kuwa miongoni mwa wagombeaji ulisema alisajiliwa kama mpiga kura muda wa usajili wa wapigakura uliowekwa na sheria ukiwa umeisha.

Wakili Ambala, ambaye anawakilisha upande huo, alisema Bw Mariga alisajiliwa mnamo Agosti 26 na hapaswi kushiriki kwenye uchaguzi huo kwani alijisajili siku 12 baada ya nafasi hiyo kutangazwa kuwa wazi.