ODM yaponda washirika ‘kuweka ushindani’ Kibra
Na VICTOR RABALLA na JUSTUS OCHIENG
CHAMA cha ODM kimelaumu washirika wake katika muungano wa Nasa, kwa kukisaliti kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra, kwa kufadhili wawaniaji wengine kwenye uchaguzi huo.
ODM ilidai kwamba vyama hivyo vinakiuka makubaliano ya muungano huo.
Ijumaa, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna aliwalaumu viongozi wa vyama vya Ford Kenya na Amani (ANC), kwa kusambaratisha muungano huo kupitia kusimamisha wawaniaji kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 7.
Alimlaumu kiongozi wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi kwa kuendeleza ajenda za wapinzani wao kisiasa.
“Uchaguzi mdogo wa Kibra huenda ukawa mtihani utakaovunja umoja wetu. Hatutawaruhusu watu wanaodai kushirikiana nasi kuyumbisha umoja huo,” alisema Bw Sifuna.
Alitoa kauli hiyo huku mbunge mmoja katika chama cha ANC akikilaumu kwa kufadhili mwaniaji katika uchaguzi huo.
ANC imemsimamisha Bw Eliud Owalo, huku Ford-Kenya ikimsimamisha Bw Khamisi Butichi.
Mbunge Maalum Godfrey Osotsi, alidai kuwa hatua hiyo ni njama ya chama hicho “kulipiza kisasi” dhidi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Bw Owalo alikuwa msimamizi mkuu wa kampeni za Bw Odinga mnamo 2013.
Bw Osotsi alisema kuwa hatua ya chama kutoandaa shughuli ya mchujo, inazua maswali kuhusu taratibu zilizotumiwa kumpa Bw Owalo tiketi ya moja kwa moja.
Kisasi
Alimlaumu vikali Bw Mudavadi, akisema kuwa amejiingiza katika siasa za ulipizaji kisasi.
Vilevile, alimkashifu vikali Katibu Mkuu wa chama hicho Bw Barrack Muluka, aliyemkosoa kuwa sababu kuu ya kushindwa kwa muungano wa Cord kwenye uchaguzi wa urais mnamo 2013.
Bw Muluka alihudumu kwa muda kama mkurugenzi mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha Bw Odinga kabla ya kuondoka.
Alisema kuwa Mabwana Owalo na Muluka bado wana machungu na Bw Odinga, ambapo wao ndio walimshinikiza Bw Mudavadi kuchukua hatua hiyo.
“Bw Mudavadi ameingizwa kwenye vita vya kisiasa dhidi ya Bw Odinga na watu wawili wenye machungu ambao walimfanyia kazi kabla ya uchaguzi wa 2013,” akasema.
Bw Sifuna alimtaka Mudavadi na Wetang’ula kujiandaa kushindwa na ODM.