• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Wanafunzi wavumbua mashine ya kuunda matofali

Wanafunzi wavumbua mashine ya kuunda matofali

NA RICHARD MAOSI

[email protected]

Mfumo wa elimu ya kisasa CBC (competence based curriculum) unahimiza wanafunzi kujipatia ujuzi sio tu wa kukabiliana na changamoto za maisha, bali pia kutegemea masomo ya vitabuni kwa faida za baadae.

Tajriba ya kazi iendane na uzoefu,ambao kwa hakika utawasaidia wasomaji wa leo,kutengeneza nafasi nyingi za ajira ili kuinua uchumi wa nchi,na kuwapatia motisha vijana waje kuwa watu wa kujitegemea.

Hii ndiyo hali halisi kutoka shule ya upili ya Sister Irene Stefani ,inayopatikana katika kaunti ya Nyandarua kilomita 15 hivi kutoka mjini Nyahururu katika barabara ya kuelekea Nyeri.

Wanafunzi kwa ushirikiano na mwalimu wao mkuu Bw Joseph Kahiga Mwangi ,walikuja pamoja na wamevumbua kifaa cha kutengeneza matofali kutokana na udongo wa kawaida uliochanganywa na saruji.

Mwalimu Joseph Kahiga akishirikiana na wanafunzi wake huku wakitumia kifaa maalum cha kutengeneza matofali bila kutegemea moto. Picha/ Richard Maosi

Bwana Kahiga anasema kidesturi watu wengi wanaojihusisha na kutengeneza matofali kwa ajili ya mauzo wanategemea moto na kuni kwa wingi.

Anaona kuwa kasumba yenyewe imekuwa ikichangia uharibifu wa mazingira, jambo linalotishia taifa kugeuka na kuwa jangwa kwa sababu ni asilimia tatu tu ya misitu iliyobakia.

“Isitoshe moshi ukiwa ni mwingi kupita kiasi,unaweza ukachafua mazingira na kusababisha maradhi ya kupumua ,”Bw Kahiga aliongezea.

Lengo lao kubwa likiwa ni kuchangia katika ulingo wa kutengeneza miundo ya kisasa taifa la Kenya linapojiandaa kufikia ruwaza ya 2030.

Mwalimu Joseph Kahiga akionyesha baadhi ya matofali yaliyotengenezwa na wanafunzi wake,yakiwa yamepakiwa huku yakisubiri kutumika. Picha/ Richard Maosi

Mwalimu Kahiga anasema alianzisha mradi wenyewe yapata miaka saba iliyopita ili kuwaandaa wanafunzi wake kimawazo, wafahamu kuwa kazi kazi ni kazi hata ile ya kuoka matofali inalipa.

Wapate mtazamo chanya kuwa binadamu anaweza kufanya kazi yoyote,badala ya kutegemea zile za ofisini ambazo ni finyu siku hizi.Aidha alitaka kuwaumbia akilini dhana kuwa enzi za kuchagua kazi zimepitwa na wakati.

“Ingawa shuleni tunafanya Building and Construction kama somo,sio wanafunzi wengi wanaopata fursa ya kutumia ubunifu wa kujitengenezea vyombo vya kurahisisha kazi,”akasema.

Shule nyingi hazijawekeza ipasavyo katika sekta ya ufundi, wala hazichukulii maanani taaluma yenyewe,ikifikiriwa kuwa hizi ni kazi duni.

Hiki ndicho kifaa kinachotumika kutengeneza matofali. Picha/ Richard Maosi

“Mataifa yaliyopiga hatua katika sekta ya utafiti na maendeleo kama vile Ufaransa,Uchina na Uingereza yanasifika kutokana na idadi kubwa ya wafanyikazi wanaosanifu miundo misingi na mijengo,”akasema.

Ikizingatiwa kuwa wanafunzi wengi wao wanatokea katika familia za hadhi ya chini,Kahiga anajibidiisha kubadilisha maisha ya baadhi yao akiamini kuwa vijana ndio nguvu kazi wa siku za mbeleni.

Utaratibu wa kutengeneza matofali

Akilimali ilitangamana na baadhi ya wanafunzi wakati wao wa mapumziko, wakitengeneza matofali, na mmoja wao ni Francis Karumi kutoka kidato cha pili.

Alieleza kuwa anatazamia kuwa mhandisi wa ujenzi na mitambo siku za baadae ili aje kusimamisha mijengo imara mijini itakayodumu kwa miaka mingi na karne.

Hatua ya kwanza wanafunzi hulazimika kukusanya mchanga wa kawaida wenye rangi iliyokolea wekundu (loam soil), na kujaza kwenye ndoo kisha wakausafirisha hadi katika karakana yao ya kazi ndani ya shule.

“Kila ndoo nne za mchanga huchukua ndoo moja ya saruji,ambapo mchanganyiko wenyewe huchanganywa vyema na kunyunyiziwa maji kidogo ili simiti na udongo ushikamane vyema,”akasema.

Idadi ya mchanga inastahili kushinda kiwango cha simiti,ili kuhakikisha matofali yanadumusha rangi ya kahawia au hudhurungi,ambayo ni maarufu miongoni mwa wajenzi na wanunuzi wengi.

Wanafunzi wakiwa kazini wakati wa kuandaa matofali. Picha/ Richard Maosi

Aidha Bw Kahiga alitufichulia kuwa hatua zote ni rahisi na za bei nafuu kwani mchanga ni mali halisia yanayopatikana katika ardhi, bila kutumia fedha zozote isipokuwa saruji ambayo huuzwa 600 mfuko mmoja.

Mchanganyiko wa saruji na udongo huingizwa ndani ya sehemu pana juu ya kifaa hiki kilichoundwa kwa umbo lenye mstatili.

Aidha huwa na sehemu ya kushikilia wakati wa kuandaa matofali,sehemu yenyewe hutumika kufinya mchanga na saruji ili kutoa matofali.

Bila kutumia nguvu nyingi kifaa chenyewe husukuma na kufinya mchanganyiko wa udongo ili kuondoa maji na kufanya mchanganyiko uwe dhabiti.

Wanafunzi shule ya Sister Irene Stefani Nyahururu wakionyesha baadhi ya matofali waliyotengeneza kutokana na mchanga pamoja na saruji. Picha/ Richard Maosi

Matofali yakiwa tayari huchomoka juu ya muundo, baada ya dakika mbili hivi na yanaweza kupakiwa katika sehemu yenye joto la kadri yakisubiri kutumika katika ujenzi.

Kahiga anasema kifaa hiki kimesaidia shule kuweka mikakati ya kutengeneza mijengo ya kisasa,ikizingatiwa baadhi ya madarasa na mabweni bado yametengenewa kwa mabati.

“Kwa kipindi cha miaka miwili ninaamini tutakuwa tumebadilisha taswira ya shule na miundo misingi kutokana na idadi kubwa ya matofali tunayowekza kutengeneza kwa siku,” alisema.

Ambapo mfuko mmoja wa saruji unaweza kutengeneza baina ya matofali 40 -50, hii ina maana kuwa endapo wangeamua kuyauza matofali wangepata baina ya 2400-3000 kutokana na mfuko mmoja wa saruji.

Ikumbukwe kuwa maji na mchanga ni malighafi ya asili yanayoweza kupatikana bila kutumia hela zozote kugharamia ,jambo linalofanya mchakato mzima kuwa nafuu zaidi.

Kahiga anaona kuwa endapo shule nyingi zinazopatikana mashinani zitakumbatia mfumo wenyewe zinaweza kutengeneza mijengo ya kisasa badala ya kutegemea serikali iwatengenezee kila kitu.

Pia anaona kuwa ni bei nafuu kwa sababu mchakato mzima hautaweza kuumiza mifuko ya wazazi wanaoitishwa hela za ujenzi na usimamizi wa shule kila mara kusanifu au kujenga madarasa na mabweni.

Kutokana na azma yake kuwahimiza wanafunzi kuzingatia umuhimu wa kutumia ubunifu wao kufanya kazi amefanikiwa kuwapeleka zaidi ya wanafunzi 57 katika matawi mbalimbali na NYS (National Youth Service ) kote nchini.

“Mbali na kushirikiana na watoto kutoka kwenye familia za wafugaji kutoka Samburu, Mararal, Laikipia, Kajiado na Narok,” akasema.

You can share this post!

Warsha ya kukabili uhalifu mijini yaandaliwa

Hatua za kuboresha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa

adminleo