Makala

DAMARIS TABBIE: Nalenga kukuza vipaji kuimarisha uigizaji Kenya

September 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

NI miongoni mwa wasanii wa kike wanaoendelea kuvumisha ulingo wa burudani ya maigizo hapa nchini. Aidha anaorodheshwa kati ya waigizaji wanaolenga kujituma mithili ya mchwa kwenye jitihada za kuhakikisha wametimiza malengo yao hasa kutinga upeo wa hadhi ya kimataifa miaka ijayo.

Anasema katika mpango mzima anapania kufuata nyayo za wasanii waliovuma katika tasnia ya filamu duniani kama Angelina Jolie mzawa wa Marekani.

Damaris Ketrai Tabbie anasema pia amepania kumiliki brandi ya kuzalisha filamu miaka ijayo huku akilenga kukuza waigizaji wanaoibukia.

Kando na uigizaji demu huyu anasema kuwa pia anajishughulisha na biashara tofauti kwenye jitihada za kusaka mkwanja kujikimu kimaisha.

Msanii Damaris Ketrai Tabbie. Picha/ John Kimwere

”Wasanii wa Kenya tunapaswa kufahamu lazima tuwe wabunifu pia tujitahidi tuwezavyo kwenye juhudi za kuzalisha kazi bora ili kupata mpenyo kama ilivyo kwa filamu za kigeni ambazo zimeibukia kuzima matumaini ya wengi wetu,” anasema na kuongeza kuwa itakuwa vyema kwa wasanii wa hapa nchini wajitume bila kulaza damu pia wafanye utafiti zaidi na kila mmoja kuwa na malengo fulani.

Anadokeza kuwa aliamini ametunukiwa talanta tosha na kuamua kuzamia zaidi masuala ya uigizaji mwaka mmoja baada ya kuanza kujituma katika ulingo huu alipotazama filamu ya mwigizaji Angelina Jolie mzawa wa Marekani iitwayo ‘Salt’.

”Bila kipendeleo wala kumpigia debe filamu hiyo ilinitia motisha zaidi hali iliyonipa ari ya kutolegeza kamba,” alisema. Ingawa tangu akiwa mdogo alidhamiria kuwa mtunzi wa nyimbo aligeukia sekta ya maigizo mwaka 2009 alipojiunga na kundi la Jicho Four Productions.

Kando na Jicho Four Productions pia mwigizaji huyu amefanya kazi na makundi mengine mengi ikiwamo Moon Beam Productions na Phil It Productions.

Anasema kuwa alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji akiwa na umri wa miaka kumi ambapo alikuwa akishiriki michezo ya kuigiza kanisani.

Kisura huyu anajivunia kushiriki vipindi kadhaa zinazoendelea kupeperushwa kupitia stesheni tofauti hapa nchini. Hushiriki: Inspekta Mwaka (Citizen TV), Kenda Imani (KBC), Auntie Boss (NTV) na Hullabaloo Estate(Maisha Magic East pia GoTV Channel 4).

Kwenye kipindi cha Kenda Imani anafahamika kama ‘Principal’ ambapo katika uhusika wake ni mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi. Demu huyu anasema kuwa anachukulia uigizaji kama ajira kwa kuzingatia ndiyo taaluma inayomsaidia kujikimu kimaisha.

Kimataifa anataja wasanii wawili ambao hutamani sana kufanya kazi nao ambao hushiriki filamu za Kinigeria (Nollywood) kama Rita Dominic na Queen Nwokoye ambao wameshiriki filamu ya ‘One room’ na ‘Banana Island’ mtawalia. Kwa wenzie hapa nchini angetaka zaidi kufanya kazi na wasanii kama Liz Nyagah na Tinsell.

Anawataka wenzie hapa nchini waache kubaguana mbali waige mtindo wa wenzao katika mataifa yanayofanya vyema kama Nigeria na Afrika Kusini ambapo kila msanii husapoti mwenzie.

Pia anatoa mwito kwa serikali isapoti sanaa ya maigizo kikamilifu bila kusuasua huku akidokeza kuwa tasnia hiyo imefurika vijana wengi wenye vipaji lakini imeibuka vigumu kwao kutambulika.