Mtihani huu wa Darasa la Tatu haueleweki, wasema wazazi
LEONARD ONYANGO na PHYLLIS MUSASIA
HALI ya kuchanganyikiwa imekumba wanafunzi 1.3 milioni wa Darasa la Tatu ambao wamekuwa wakijiandaa kufanya mjarabu wa kitaifa uliotarajiwa kuanza Jumatatu, huku Wizara ya Elimu ikishikilia kuwa hakuna mtihani.
Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang jana alisema wanafunzi wa Darasa la Tatu wanaendelea na masomo yao ya kawaida na wala hawafanyi mtihani.
Hii ni licha ya kuwa katika shule mbalimbali za msingi kote nchini, wanafunzi walionekana wakijiandaa kwa mjarabu huo.
“Hakuna mtihani unaoendelea shuleni kwa sasa. Tunachofanya ni kukagua namna wanafunzi wanaendelea kimasomo na tutaandaa ripoti ya pamoja itakayotuwezesha kubuni sera zifaazo,” akasema Dkt Kipsang aliyekuwa akizungumza alipozuru shule ya Msingi ya Moi Avenue, Nairobi.
Alisema shughuli ya kutathmini wanafunzi wa Darasa la Tatu itaendelea hadi mwisho wa muhula wa pili,” akasema.
Wanafunzi hao ambao ni wa kwanza kusoma Mtaala Mpya wa Elimu (CBC) watatathminiwa katika masomo ya Hisabati, Kiingereza na Kiswahili.
Dkt Kipsang alisema hayo huku wanafunzi jana walikuwa wakifanya maandalizi yao ya mwisho kwa ajili ya mtihani huo.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo, ulibaini kwamba wanafunzi wa Darasa la Tatu jana walikuwa wakifanya maandalizi ya mwisho wakijiandaa kufanya mtihani wa Hisabati.
Katika shule ya Msingi ya Green Mount Kakamega wana tulipata wanafunzi wakifanya maandalizi kabambe.
Wazazi wa wanafunzi wa Darasa la Tatu waliozungumza na Taifa Leo katika Kaunti ya Nakuru walisema kwamba hawakuwa na ufahamu kuhusu mambo yatakayofuata baada watoto wao kufanya mtihani huo.
“Ni kweli kwamba tumewasaidia wanafunzi wetu kufanya maandalizi ya mtihani huo ambao ni wa kwanza kuwai kufanyika nchini chini ya Mtala Mpya wa Elimu (CBC) lakini hatuna uhakikika ikiwa huo ndio utakao kuwa mwisho wa masomo ya muhula huu,” akasema Bi Ann Wanjohi.
Mzazi mwingine, Bw John Moses Kimani alisema shule imekuwa ikihusisha wazazi kwenye maandalizi ya mtihani huo hata ingawa wazazi walilazimika kukaa karibu na wanao ili kuwasaidia kuelewa mambo mengine.
Makanisa mbalimbali yaliombea wanafunzi wa Darasa la Tatu ili waweze kufanya vyema katika mtihani wao.
Lakini Dkt Kipsang alisema ripoti ya utathmini huo haitatumiwa kuorodhesha shule au wanafunzi waliofanya vyema.
“Ripoti hiyo haitatumiwa kuteua wanafunzi watakaojiunga na Darasa la Nne. Watoto wote walio katika Darasa la Tatu wataenda katika Darasa la Nne mwaka ujao,” akasema Dkt Kipsang.
Alisema wiki ijayo wizara ya Elimu itazindua rasmi silabasi ya Darasa la Nne.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi ya Moi Avenue Lucy Chirchir alisema hakuwa na habari kuhusu mtihani.
“Ninachofahamu ni kwamba Wizara ya Elimu ilitutumia vifaa vitakavyotumiwa katika utathmini wa wanafunzi. Sasa ni jukumu la mwalimu wa somo husika kupanga siku ambayo atathimini wanafunzi,” akasema Bi Chirchir.
“Kwa mfano, kama ni kusoma kwa sauti, mwalimu atahakikisha kuwa wanafunzi wote wamesoma na hiyo huenda ikachukua hata wiki mbili kulingana na idadi ya wanafunzi,” akaongezea.