Habari Mseto

Watu 6 waangamia katika ajali ya Mazeras

September 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MISHI GONGO na MAUREEN ONGALA

WATU sita walifariki Jumatatu katika ajali mbaya ya barabarani iliyotekea sehemu ya Makobeni Kaloleni katika barabara kuu ya Mazeras.

Ajali hiyo iliyotokea saa tatu asubuhi ilihusisha trela mbili, basi la abiria na magari mengine kadhaa ya kibinafsi.

Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Kilifi Bw Patrick Okeri alisema magari hayo yalikuwa yakielekea pande tofauti ikiwemo Mombasa na Nairobi.

‘Dereva wa trela moja alikuwa akiendesha kiholela na akagongana ana kwa ana na gari jengine lililokuwa likitoka Mombasa, kulikuwa na magari mengine ambayo pia yalikuwa yakiendeshwa kwa mwendo wa kasi hivyo kushindwa kusimamisha gari kwa ghalfa hivyo kugonga magari yalokuwa yamegongana,’ alisema.

Kamanda huyo alisema wengi wa walionusurika hawakuhitaji msaada wa kutolewa ndani ya magari waliyokuwemo kwani walipata majeraha madogo.

Akizungumza na Taifa Leo, mwanamke aliyeshuhudia tukio hilo na aliyetaka jina lake kubanwa alisema ajali hiyo ilisababishwa na trela lililokuwa likitoka kaloleni lilipokuwa linajaribu kukwepa gari la kibinafsi lililokuwa limeegeshwa, hivyo kupoteza mwelekeo na kugongana na basi la abiria lililokuwa likitoka Mombasa mjini.

‘Magari yetu yalikuwa yamekwaruzana hivyo tukasimama ili kusuluhisha,wakati huo ndiyo trela lililokuwa likitoka Kaloleni lilikuwa linakuja na mwendo wa kasi,lilijaribu kupita magari yaliyokuwa yameegeshwa na hapo ndiyo liligongana na basi dogo lililokuwa katika Mombasa,’ alieleza.

Mwingine aliyeshuhudia, Bw George Chenza alisema trela lililokuwa likitoka Kaloleni lilikuwa limebeba mchanga wa kujengea.

‘Mbali na sita waliofariki, wengi waliokuwa kwa magari hayo walijeruhiwa. Walipelekwa katika kituo cha afya na wasamaria wema’ alisema Bw Chenza.

Miili ya waliofariki ilipelekwa katika hospitali kuu ya rufaa ya mkoa wa Pwani almaarufu kama Makadara.