Makala

SHINA LA UHAI: Taswira ya vifo vya uzazi na watoto wachanga nchini Kenya

September 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na BENSON MATHEKA

IDADI ya watoto wanaofariki wakati wa kuzaliwa na kabla ya kutimiza miaka mitano na akina mama wanaoaga dunia kutokana na matatizo wakati wa kujifungua nchini inasikitisha japo imepungua katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Tafiti za hivi punde zinaonyesha kuwa vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 30 katika kipindi cha miaka saba iliyopita ikiwa ni watoto 34,000 wanaokufa kila mwaka.

Kulingana na utafiti wa kutathmini hali ya afya nchini (Kenya Demographic Health Survey-KDHS 2014), kupungua kwa vifo vya watoto kunatokana na wanawake kukumbatia mpango wa uzazi, mbinu bora za kulisha watoto, kuzuia Malaria, kukabiliana na Ukimwi na kutolewa kwa chanjo.

Aidha, wataalamu wa afya wanasema wanawake wengi wameanza kujifungulia katika vituo vya afya baada ya serikali kuondoa malipo na kurahisisha upatikanaji wa bima ya matibabu.

“Vifo vya watoto vilipungua hadi 39 kwa kila watoto 1000 waliozaliwa 2014 kutoka 52 ilivyokuwa 2008 na 2009. Aidha, idadi ya watoto wanaokufa kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano ilipungua hadi 52 kwa kila watoto 1000 mwaka huo kutoka 74 ilivyokuwa 2008 na 2009,” unaeleza utafiti huo.

Kulingana na hazina ya Umoja wa Mataifa kuhusu watoto (UNICEF), watoto 46 kati ya 1000 walifariki kabla ya kutimiza miaka mitano nchini Kenya 2017.

Kwa jumla, Unicef inasema watoto 68,882 walifariki nchini Kenya mwaka huo kabla ya kufikisha miaka mitano. Kote ulimwenguni, watoto 2.7 milioni walikufa mwaka huo kabla ya kufikisha miaka mitano.

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa idadi hiyo imekuwa ikipungua pakubwa kutoka mwaka wa 1990 ilipokuwa asilimia 110.

Utafiti huo ulinuiwa kupata habari za kusaidia kupanga, kutekeleza na kufuatilia mahitaji ya kiafya, mpango wa uzazi na miradi ya kukabiliana na Ukimwi.

Wataalamu wa afya ya watoto wanakiri kuwa kupungua kwa vifo vya watoto kunatokana na matumizi ya neti za kukinga mbu, kuimarika kwa huduma wanazopata akina mama wajawazito ikiwa ni pamoja na akina mama kujifungua wakisaidiwa na wakunga waliohitimu.

“Kuna mabadiliko makubwa kwa sababu wanawake wengi wanapata huduma katika hospitali wakiwa na mimba na wakati wa kujifungua. Hii imesaidia kupunguza vifo vya watoto na hata akina mama wakati wa kujifungua,” asema mtaalamu wa afya ya watoto, Dkt Seth Nanjala.

Uzani mdogo

Kulingana na utafiti, idadi ya watoto wanaozaliwa wakiwa na uzani wa chini imepungua kwa sababu ya akina mama kupata lishe bora.

Aidha, idadi ya watoto wanaokosa kukua vyema kutokana na lishe duni ilipungua kutoka asilimia 35 hadi 26 kati ya 2009 na 2014 huku idadi ya watoto walio na uzani wa chini ikipungua kutoka asilimia 16 hadi 11.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 59 ya watu nchini Kenya wanatumia neti za kukinga mbu, hii ikiwa ni zaidi ya nusu ya watoto wote walio na umri wa chini ya miaka mitano na nusu ya wanawake walio na mimba.

Kulingana na ripoti ya KDHS 2014, vituo vya afya viliongezeka kwa asilimia 61 kutoka asilimia 43 ilivyokuwa 2008 huku asilimia 80 ya wanawake na asilimia 71 ya wanaume wakijitolea kupimwa Ukimwi. Hii inahusishwa na kugatua huduma za afya.

Wataalamu wanasema kwamba licha ya hatua hizo kupigwa, watoto wengi hufariki kutokana na malaria, kuhara, utapia mlo na nimonia.

Dkt Nanjala anasema kwamba vifo vya watoto kutokana na malaria vinaweza kuepukwa kwa kuhakikisha wanalala chini ya neti ya kujikinga na mbu.

“Maradhi kama nimonia yanaweza kuepukwa kwa kunyonyesha mtoto vyema hadi afikishe umri wa miaka miwili na kuhakikisha nyumba wanayolala ina hewa safi. Watu wengi huwa wanahatarisha maisha ya watoto kwa kukosa kuwanyonyesha vyema na hilo hudhoofisha afya yao,” asema.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa watoto wanapaswa kunyweshwa maji safi na salama kila wakati ili kuwaepusha na maradhi ya kuhara.

“Mazingira anayowekwa mtoto yanafaa kuwa safi, apewe chakula safi na bora ili kuepuka utapia mlo,” akasema.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), chanjo kwa mtoto ni muhimu ili kumkinga na hatari ya maradhi. Shirika hilo linasema kwamba watoto wengi hufa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiliwa na kutibiwa.

Kunyonyesha ni njia ya pekee ya kuhakikisha mtoto anakua akiwa na afya na kuendelea kuishi, linasisitiza shirika hilo.

Kulingana na WHO, kama viwango vya kunyonyesha vingekuwa vya hali ya juu duniani, takriban maisha 820 000 ya watoto yangenusurika kila mwaka.

Aidha ripoti ya UNICEF inasema kuwa malaria huchangia asilimia 18 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano katika ba?a la Af?ika. Magonjwa ya kuhara na nimonia yanachangia asilimia 40 ya vifo vya watoto.

Kulingana na Dkt Nanjala, mjamzito kuhudhuria kliniki inavyostahili hupunguza hatari ya mtoto kufa baada ya kuzaliwa.

“Wakati anapohudhuria kliniki, mama na mtoto hufanyiwa uchunguzi na kushauriwa ipasavyo. Kukosa kuhudhuria kliniki kunaweka mama na mtoto kwenye hatari zaidi,” aeleza.

Wataalamu wanashauri wazazi kuwapeleka watoto wao ambao hawajafikisha umri wa miaka mitano kliniki kila mwezi.

“Inafaa mtoto achunguzwe hadi afikishe miaka mitano,” aeleza Dkt Daniel Kibe wa hospitali ya Bristol, jijini Nairobi.

Anasema watoto wengi hufariki kwa kutopata lishe bora.

“Lishe bora ni muhimu katika kujenga kinga ya mwili na hivyo ni muhimu kuhakikisha kwamba watoto wanapata lishe bora kwa ajili ya kusaidia kuepuka magonjwa ambayo yanaweza kuzuiliwa,” asema.

Ugumu wa kupata chakula

WHO inasema kuwa upatikanaji wa chakula cha kutosha na bora bado ni changamoto katika mataifa mengi maskini.

“Ili kuweza kuzuia vifo vya watoto, lishe ni mojawapo ya masuala muhimu katika jitihada za kufikia lengo la nne la yaliyokuwa malengo ya maendeleo ya milenia. Hata hivyo lishe bora bado ni changamoto katika mataifa mengi,” inaeleza WHO.

Watetezi wa afya katika jamii wanasema licha ya Kenya kupiga hatua katika kupunguza vifo vya watoto wachanga, serikali inapaswa kuepusha migomo ya wahudumu wa afya.

“Migomo ya mara kwa mara ya wahudumu wa afya imechangia vifo vya watoto na akina mama wanapokosa kupata huduma ifaayo. Ikiwa Kenya inataka kuingia katika orodha ya nchi zilizokabiliana na vifo vya watoto wachanga, inafaa kumaliza mizozo na wahudumu wa afya,” anaeleza Doris Wakio, mtetezi wa afya na mshirikishi wa shirika la Afya Bora Coalition.

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Nchini (Kemri), asilimia 75 ya watoto hufa wakati wa kuzaliwa (neonatal deaths) hii ikiwa ni watoto 22 kwa kila watoto 1000 idadi ambayo watetezi wa afya wanasema inaweza kupunguzwa iwapo mizozo itaepukwa.

Bi Wakio anasema mama anapochukua muda mrefu kabla ya kujifungua, ndivyo hatari ya mtoto kufa inavyoongezeka.