GSU, Pipeline mabingwa wa voliboli
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Kenya General Service Unit (GSU) na Kenya Pipeline ziliteremsha voliboli safi dhidi ya wapinzani wao na kutawazwa wafalme na malkia katika mashindano ya kuwania taji la wazi yaliyofanyika mjini Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.
Pipeline ilitwaa taji hilo baada ya kutandika mahasimu wao Kenya Prisons seti 3-2 (25-23, 25-23, 23-25, 18-25, 15-07) katika fainali.
Kwenye ngarambe hiyo, Pipeline na Prisons zilikosa huduma za Janet Wanja na Jane Wacu mtawalia ambao ni miongoni mwa maseta mahiri nchini.
Wawili wamo katika timu ya taifa maarufu, Malkia Strikers inayoshiriki katika fainali za voliboli ya Kombe la Dunia (FIVB) nchini Japan.
Pipeline ilikomoa mahasimu hao baada ya kuwanyuka seti 3-2 kwenye mechi za Ligi Kuu ya KVF uwanjani humo. Katika fainali ya wanaume, GSU ilikandamiza mahasimu wao Kenya Prisons kwa seti 3-1 (25-15, 23-25, 26-24, 25-16).
”Nawashukuru wachezaji wa Pipeline kwa kutwaa taji hilo baada ya kulemea wapinzani wao wakuu,” alisema meneja wake, Kassuja Onyonyi na kuongeza kuwa vipusa hao bado wanaweza kukazana na kufanya bora zaidi.
Kwenye nusu fainali, GSU ililaza Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) set 3-1 (25-13, 24-26, 25-20, 25-21) nayo Kenya Prisons ilisajili seti 3-2 (25-23, 15-25, 25-17, 17-25, 15-11) mbele ya Equity Bank.
Upande wa wanawake, KCB ilinyukwa seti 3-1(17-25,25-17, 26-24, 25-18) na Pipeline nayo Directorate of Criminal Investigations (DC1) ilibanwa seti 3-1 (25-15, 20-25, 25-21,25-14) na Kenya Prisons.