• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
WASIA: Tusiwashinikize wanafunzi kupata matokeo zaidi ya uwezo wao

WASIA: Tusiwashinikize wanafunzi kupata matokeo zaidi ya uwezo wao

Na HENRY MOKUA

UMEWAHI kupewa zoezi fulani la kuchukua saa chache ukajiambia kwamba utatenga saa hizo baadaye kulikamilisha kisha ukalikumbuka saa chache kabla ya makataa?

Kwa kawaida inapofanyika hivyo, unakuwa mwepesi wa kulifanya japo makosa ya hapa na pale hayakosekani. Kwa kweli, tunaweza kusema kwamba unapolazimika au kushinikizwa kulifanya jambo fulani, unakuwa mwepesi wa kulifanya.

Ni mambo mengi tuliyoyafanikisha kwa jinsi hii hata yakawa mazoea yetu kwamba ukitaka mtu akamilishe kazi kwa wakati, sharti umsukume kidogo. Ilivyo ada lakini, kila jambo lisilotendwa kwa kiasi huwa na madhara ambayo yaweza kubatilisha manufaa yote ya awali ya jambo hilo.

Wapo wazazi na walimu wanaosahau kwamba shinikizo zina wakati wake na kiasi cha kuwa na manufaa.

Nasema hivi kwa sababu wanafunzi fulani walinijia majuzi wakashtakia namna wazazi wao wanavyowashinikiza kutimiza matazamio yao katika mitihani ya kitaifa inayokaribia.

Wazazi na walimu hawa, licha ya kujua uwezo wa wanafunzi husika, wanatarajia kwamba kwa sababu binadamu ni mvivu, kwa kawaida inabidi watumie mbinu hii ili wanafunzi hao wafuzu vilivyo.

Ewe mwalimu na mzazi unayefikiri hivi, naomba uone hatari inayokukodolea macho ili uchukue hatua ya dharura kuibatilisha.

Kwa kumshinikiza mwanao afikilie matokeo asiyoweza kuyafikilia, unamkatiza tamaa.

Ni kwa msingi huu tunashauri kila mara kwamba wakati wa kujiwekea shabaha, mwanafunzi hupaswa kujikadiria vilivyo kwani akijiwekea shabaha ya chini, huanza kuwa mzembe kwani huhitaji juhudi kidogo tu kutimiza shabaha yake.

Aidha, ni hatari akijiwekea shabaha ya juu mno, hukata tamaa kwa kujiambia: heri nisijisumbue, sitapafikia pale!

Tokeo la kauli hii ni kwamba atasalia kama asiye na shabaha yoyote na hivyo kuishia kuyafanya mambo yake kikawaida tu. Kumbuka shabaha hunuiwa kumhamasisha mwanafunzi ili ajitahidi zaidi; ikigeuka kuwa kisa na sababu ya kumpotezea tumaini, heri isiwepo.

Ajabu nyingine ya kumshinikiza mwanao, hasa mtahiniwa ni kwamba anaona badala ya kukosa shabaha yako – si yake tena – kwa kiasi kidogo kisha matokeo yawe yale yale ya kudhalilishwa na labda kusimangwa, heri afeli vilivyo. Kwa hivyo hata kutulia kusoma ni suala litakalomtatiza kwani ataona hajasoma lolote hata ambapo amesaza masuala machache tu.

Aidha, shinikizo iliyokiuka mpaka ni chanzo cha uhusiano mbaya kati ya mwenye kushinikiza na mwenye kushinikizwa.

Kumtaka mwanao au mwanafunzi wako afikilie matokeo yanayopiku uwezo wake ni namna ya kumfanya ajihisi kwamba hajawa bora kiasi ukitakacho iwapo hajapata matokeo uyatakayo. Ikisadifu kwamba yupo mwenziwe ambaye amefanikiwa kutimiza malengo yake, ya mzazi wake japo yapo juu, hujiona asiyefaa na hivyo kusalia kufikiri humthamini.

Kukata tamaa kwa sampuli hii ni tukio hatari unalopaswa kujiepusha nalo. Baadhi ya wanafunzi walioripotiwa kujitia kitanzi kwa miaka michache iliyopita waligunduliwa kufikia uamuzi wao potovu shinikizo ikiwa mojawapo ya sababu zao kuu.

Chukua hatua ya mapema kumwondoa mwanao katika orodha hiyo ndefu.

Ikiwa nimekwisha kukosea kwa kuchukua hatua hii ya kumshinikiza mwanangu au mwanafunzi wangu kupindukia nifanyeje?

Hatua ya busara ya kuchukua ni kutenga muda, kuketi na mwanao na kumhimiza. Yakiri mambo aliyoyafanya vilivyo hadi sasa, ya kiakademia na ya jumla.

Kisha mtajie machache unayoona yana uwezo wa kumwangusha mtihani. Mweleze ulivyo na imani kwake na kumtaka atie bidii kadri ya uwezo wake kisha akutajie msaada anaoutaka kwako na anaoona una uwezo wa kumpa.

Mpongeze kwa kila hatua ndogo anayoipiga ili ajiamini kwani bila kujiamini, hapana la mno la kutarajia. Akiridhika kwamba watu wa karibu, hasa wazazi wake wanamwamini na wataridhishwa na matokeo ya bidii yake, atajituliza, kujituma na kufanya kazi itakayokushangaza hata wewe!

You can share this post!

MAPITIO YA TUNGO: ‘Naomba Unisamehe’ ni novela...

VITUKO: Msodai apeleka wanafunzi Pwani badala ya shambani...

adminleo