MAPISHI: Namna ya kupika minofu ya kuku iliyotiwa asali
Na MARGARET MAINA
ULAJI wa nyama ya kuku una manufaa mengi kwa mwili wa binadamu.
Husaidia upatikanaji wa virutubisho muhimu vya siku kwani nyama nyeupe ina mafuta kidogo, vitamini, protini na nguvu kwa ajili ya shughuli za kila siku.
Aidha, nyama nyeupe huwa na amino acids nyingi ambazo ni muhimu kwa ujenzi wa seli za binadamu na ukuaji wa nywele kwa ujumla.
Nyama hizi zina mafuta kidogo sana ambayo sio hatari kwa afya ya moyo na mfumo mzima wa mwili wa binadamu.
Muda wa kuandaa: Dakika 15
Muda wa mapishi: Dakika 25
Walaji: 3
Vinavyohitajika
- Nyama ya kuku kilo 1
- Asali vijiko 4
- Sukari ya kahawia kijiko 1 na nusu
- Soy sauce nusu kikombe
- Tangawizi vijiko 2
- Kitunguu saumu
- Sosi ya chili vijiko 3
- Chumvi
- Udaha yaani cayenne pepper kiasi
- Mafuta ya mizeituni vijiko 5
- Currypowder kijiko 1
- Coriander powder kijiko 1
- Ndimu 1
Maelekezo
Changanya pamoja sukari, asali, soy sauce, tangawizi, kitunguu saumu na chilli sauce kwenye kibakuli kidogo.
Safisha kuku, kausha maji, kata minofu vipande vidogovidogo na uviweke kwenye kikaangio. Nyunyizia chumvi, cayenne pepper na juisi ya ndimu kiasi.
Weka mafuta ya kukaangia kwenye kikaangio na weka mekoni kisha weka kuku na anza kugeuzageuza kuku mpaka mafuta yapate moto, usiache kugeuza mpaka minofu ya kuku iwe na rangi ya kahawia.
Weka viungo vilivyobaki curry powder na coriander powder na koroga kwa dakika tano.
Mwisho, mwagia sosi uliyoandaa; usifunike. Pika hadi sauce iwe nzito.
Epua nyama ya kuku pakua na ufurahie na chochote ukipendacho.