• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Kitengela ni mahangaiko tele ya maji

Kitengela ni mahangaiko tele ya maji

Na SAMMY WAWERU

KITENGELA inapatikana katika Kaunti ya Kajiado na ni eneo linalokua kwa kasi hasa kwa sababu ya mradi wa reli ya kisasa (SGR) uliopita hapo.

Mradi huo umevutia wawekezaji wengi na kusababisha bei ya mashamba kupanda mara dufu.

Unapozuru mji wa Kitengela, utakaribishwa na shughuli mbalimbali za biashara, zile ya tuktuk na bodaboda zikionekana kunoga.

Serikali ya Kaunti ya Kajiado inaoongozwa na Gavana Joseph Ole Lenku, imeweka mikakati kabambe katika sekta ya usafiri na uchukuzi ambapo kila wahusika kuanzia tuktuk, pikipiki na matatu wana mahala maalum kuchapa kazi.

Licha ya maendeleo hayo, uhaba wa maji ni suala linalohangaisha wakazi usiku na mchana. Raslimali hii muhimu maishani eneo la Kitengela imekuwa dhahabu kupatikana, wakazi wakilazimika kufukua zaidi mfukoni kuigharamia.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Taifa Leo maji safi ya mtungi wa lita 20 yanauzwa zaidi ya Sh30.

Baadhi ya wakazi tuliozungumza nao wanasema bei hiyo hata ni nafuu ikilinganishwa na msimu wa kiangazi.

“Hiyo ni gharama ya kununua pekee, hujaongeza ya kusafirisha. Wakati wa ukame, mtungi mmoja haupungui Sh50,” akasema Sara Nesh wakati wa mahojiano.

Ili kupunguza gharama, mkazi huyo alisema hulazimika kubeba maji ya kukata kiu kutoka kampuni anayofanyia kazi, kilomita tatu hivi kutoka mahali anakoishi.

Kwa wenye familia hususan watoto, ni mahangaiko tele ikizingatiwa kuwa lazima wale, wanywe na wavalie nadhifu.

“Kwa siku hutumia zaidi ya Sh300 kununua maji pekee. Kwenye kiasi hicho familia yangu haijapata chakula. Tunapitia taabu chungu nzima za maji,” akalalamika mkazi anayeishi katika nyumba ya kukodi.

Baadhi ya majengo ya kupangisha yana maji ingawa kodi nayo haikamatiki. Walioondoa gharama ya maji kwenye kodi, wanauzia wapangaji.

“Mtungi mmoja wa maji yenye uchachu wanatuuzia Sh5. Hayo ni ya usafi pekee,” mpangaji mmoja akasema.

Baadhi ya malori huchuuza maji safi lakini wakazi wanalalamikia ni ghali, ikikumbukwa kuwa gharama ya maisha inaendelea kupanda kila uchao.

Uhaba wa maji Kitengela unajiri licha ya serikali ya kaunti ya Kajiado mwaka 2018 kubuni bodi ya maji, Tanathi, inayojukumika kuangazia suala la maji.

You can share this post!

‘Kuna wanawake wachache ngazi za uamuzi muhimu...

Sonko kupokea kiwango cha juu cha fedha huku Fahim Twaha...

adminleo