Habari Mseto

Nema yavitaka vituo vya afya kufuata utaratibu muhimu katika utupaji majitaka

September 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

MAGDALENE WANJA

VITUO  vyote vya afya vitatarajiwa kuzingatia taratibu na kanuni muhimu zilizowekwa kuhusu ubora wa maji, za mwaka 2006 la sivyo vitafungwa na serikali.

Kulingana na kaimu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira (Nema), Bw Mamo Boru, vituo vyote vya afya ambavyo vinachangia pakubwa katika uchafuzi wa mazingira havitaruhusiwa kutoa huduma.

Kulingana na sheria hiyo ya mwaka 2006, hakuna yeyote anayeruhusiwa kuachilia majitaka kutoka kwa viwanda ama majengo yoyote bila ya kuwa na leseni kutoka kwa Nema.

Sheria hiyo pia inahitaji majitaka kutibiwa kabla ya kuelekezwa kwenye mtaro wa kuyasafirisha.

Jana Jumatano, Nema ilifunga kituo cha afya mjini Ngong kwa madai ya kuyatupa majitaka bila kuzingatia afya na usalama wa wakazi.

Kituo hicho; Trinity Care Centre chenye vitanda 10 kilipatikana kukiuka sheria kama vile kuhudumu bila leseni za utupaji taka.

Majitaka. Picha/ Magdalene Wanja

“Tulitembelea eneo hili kufuatia mallamishi ya wakazi kuhusu maji taka kutoka kwenye kituo hicho cha afya,” alisema Bw Boru.

Bw Boru alisema kuwa baada ya wakaguzi kutembelea eneo hilo, walipata kuwa madai hayo yalikuwa ya ukweli.

Mmiliki wa kituo hicho Bw Joseph Ndaba kwa upande wake alisema kuwa alikuwa na mkataba na serikali ya Kaunti ya Kajiado ambapo anawapelekea taka ili kuharibiwa kwa mashine.

Alisema kuwa alitumia gari lake kusafirisha takataka hadi kwenye maeneo ya kuharibiwa.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Nema, Bw Mamo B. Mamo akiwa na maafisa na wakaguzi wa mamlaka hiyo. Picha/ Magdalene Wanja