• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Wabunge waliodaiwa kuchochea chuki waachiliwa

Wabunge waliodaiwa kuchochea chuki waachiliwa

NA RICHARD MUNGUTI

WABUNGE wanne walioshtakiwa kwa uchochezi waliachiliwa Alhamisi na mahakama ya Nairobi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibisha kesi dhidi yao.

Wanne hao Junet Mohammed (Suna Mashariki), Bi Aisha Jumwa (Mbunge Malindi), Bi Florence Mutua (Mwakilishi Mwanamke wa Busia) na Bw Timothy Bosire (Mbunge wa zamani Kitutu Masaba) waliachiliwa na hakimu mkuu Martha Mutuku.

Wanne hawa ni miongoni mwa wabunge sita almaarufu “ Pangani Six” walioshtakiwa kwa madai ya uchochezi na chuki cha kikabila.”

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma alisema kuwa washtakiwa kwa lengo la kuzua uhasama baina ya jamii mbali mbali nchini.

Wengine walioshtakiwa pamoja ni Bw Moses Kuria (Gatundu Kusini) na aliyekuwa Mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu ambaye sasa ni Gavana wa Kiambu.

Sita hawa walifikishwa Juni 17, 2016 baada ya kukesha katika kituo cha polisi cha Pangani kwa siku moja.

Bw Kuria na Bw Waititu walichaguliwa kwa tikiti ya chama cha Jubilee ilhali hao wengine walikuwa wamechaguliwa kwa muungano wa vyama vya upinzani Cord.

Wabunge hawa walikanusha shtaka dhidi yao licha ya kushtakiwa kwa vikundi viwili huku Mabw Waititu na Kuria wakishtakiwa mbele ya Bi Charity Oluoch.

Bi Oluoch aliwaachilia wawili hao akisema “ upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yao.”

Nao Junet, Jumwa, Mutua na Bosire walifunguliwa mashtaka mbele ya hakimu mkuu Bi Martha Mutuku.

Akiwaachilia wanne hao, Bi Mutuku alisema amechambua ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka na kufikia uamuzi kwamba “ hakuna ushahidi wa kutosha uliowasilishwa unaowezesha mahakama kuwaweka kizimbani kujitetea.”

Bi Mutuku aliongeza kusema cheti cha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao wanne hakikueleza bayana makosa waliyofanya wabunge hao.

“ Cheti cha mashtaka hakieleweki. Hakijaeleza kwa uwazi wanachodaiwa kufanya washtakiwa hawa wanne,” alisema Bi Mutuku.

Hakimu alisema sheria inasema ikiwa mmoja atafunguliwa mashtaka lazima yaeleze makosa anayodaiwa kufanya.

Alisema ikiwa cheti cha mashtaka hakisimulii makosa waliyofanya wanasiasa hao hana budi “ ila kuwaachilia.”

Hakimu aliamuru washtakiwa warudishiwe dhamana walizokuwa wameweka mahakamani.

Na wakati huo huo Gavana Waititu aliwasilisha ombi kwa hakimu mkuu Francis Andayi amruhusu awasilishe dhamana badala ya dhamana ya Sh15milioni alizolipa ndipo aachiliwe katika kesi ya kashfa ya Sh588milioni dhidi yake.

Bw Waititu ameshtakiwa pamoja na mkewe Susan Wangari kwa ulaghai wa Sh50milioni.

  • Tags

You can share this post!

Soka inavyotumiwa kuzima uhalifu

Harambee Starlets kukabiliana na Black Queens ya Ghana...

adminleo