• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Mariga atikisa handisheki

Mariga atikisa handisheki

Na LEONARD ONYANGO

MUAFAKA wa maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, maarufu kama handisheki umekumbwa na dhoruba kufuatia hatua ya kiongozi wa nchi kumuidhisha mwaniaji wa ubunge wa Jubilee katika eneobunge la Kibra, McDonald Mariga.

Baadhi ya viongozi na wafuasi wa ODM wameelezea hofu yao kuwa uhusiano kati ya viongozi hao wawili huenda ukazorota zaidi endapo Rais Kenyatta atajitosa katika kampeni za Bw Mariga.

Jana, katika hali ambayo wadadisi wanaona imelenga kumhakikishia Bw Odinga na wafuasi wake kwamba handisheki ingali imara, Mbunge Maalumu wa Jubilee Maina Kamanda alimtembelea waziri huyo mkuu wa zamani afisini mwake Nairobi na kutangaza ataunga mkono Benard Okoth almaarufu Imran, anayepeperusha bendera ya ODM kwenye uchaguzi huo.

Bw Kamanda huchukuliwa kama kiongozi wa kikundi cha Kieleweke kinachojumuisha wanasiasa wa Jubilee ambao wanashabikia handsheki wakimpinga Naibu Rais William Ruto.

“Chama cha Jubilee kimesimamisha mwaniaji wake, lakini mimi nitaunga mkono Bw Okoth wa ODM. Huyu ndiye mwaniaji wa handisheki. Hii ni kwa sababu handisheki imeleta amani nchini na watu wanafanya biashara bila wasiwasi,” akasema Bw Kamanda katika afisi ya Bw Odinga iliyoko jumba la Capitol Hill, Nairobi.

Akizungumza baada ya mkutano wao, Bw Odinga aliepuka kusema wazi kama mwafaka wake na Rais uko mashakani bali akasema Bw Kamanda alimtembelea ili kumfahamisha kuhusu hatua ambazo zimepigwa katika kupigia debe handisheki na BBI jijini Nairobi na katika maeneo mengine nchini ikiwemo Mlima Kenya.

“Tumekuwa tukishirikiana naye (Bw Kamanda) katika kupigia debe BBI ili kuhakikisha kuwa inakubalika katika pembe zote za nchi,” akasema Bw Odinga.

Lakini wachanganuzi wa masuala ya siasa wanasema, hatua ya Bw Kamanda sasa imeonyesha wazi kampeni za Kibra zitakuwa mashindano baina ya wanaounga handisheki na wanaopinga, na hivyo basi kushusha pumzi kwa Wana-ODM wanaohofia kuhusu hatima ya maelewano kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta.

Viongozi wengine wa Jubilee ambao awali walikuwa tayari wameonyesha kuchukizwa kwao na hatua ya kusimamisha mgombeaji Kibra ni Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo anakiri kuwa handisheki itakuwa taabani ikiwa Rais Kenyatta na Bw Odinga watakabiliana kwenye kampeni za kupigia debe wagombeaji wa vyama vyao Kibra.

“Ninaamini Bw Ruto na wanasiasa wa kundi la Tangatanga walimwekea mtego Rais Kenyatta, hivyo kumlazimu kutangaza kumuunga mkono Bw Mariga,” akasema Dkt Amolo.

“Tunachosubiri kuona ni ikiwa Rais Kenyatta ataongoza msururu wa kampeni kumpigia debe Bw Mariga na upande mwingine pia Bw Odinga aendeshe kampeni kwa ajili ya Imran. Hilo litazua wasiwasi,” akaongezea.

Mbunge huyo wa ODM, hata hivyo, anatumai maazimio ya handisheki ikiwemo utekelezaji wa ripoti ya BBI inayosubiriwa, utatimizwa kikamilifu licha ya uchaguzi huo mdogo unaoibua kiwewe.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alieleza wasiwasi wake kwamba, huenda Bw Odinga alihadaiwa kuweka muafaka na Rais kwani kufikia sasa, maazimio aliyolenga hayajapatikana isipokuwa kuwepo utulivu nchini.

“Baba (Bw Odinga) anafaa kujihadhari na hiki kitu kinachoitwa handisheki. Rais Kenyatta anafaa kuwa mkweli na hii handisheki. Hatutaki kudanganyana na kisha wanakuaibisha,” akaonya.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM Junet Mohamed, alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza wa ODM kueleza hisia zao wakati Bw Mariga alifikishwa Ikuluni mnamo Jumatano.

Akimjibu Dkt Ruto wakati aliweka picha ya Rais akimvisha kofia Bw Mariga kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Bw Mohamed alisema: “Nisikusikie tena vijijini ukidai Raila anavunja Jubilee, na kwamba handisheki na BBI zinahusu siasa za 2022.”

Kimsingi, alionekana kumaanisha Naibu Rais ndiye anagawanya chama hicho zaidi kwa kumsimamisha mgombeaji Kibra ambako ni ngome ya ODM kisiasa. Licha ya hayo, Bw Mohamed jana alisema Bw Kamanda na Bw Odinga wana ushawishi mkubwa kwa siasa za Nairobi hivyo basi wako imara.

“Kila mtu ana haki ya kuunga mkono mwaniaji anayetaka lakini ukweli ni kwamba, chama cha ODM kitahifadhi kiti hicho kwa urahisi,” akasema Bw Junet.

Mara baada ya Rais Kenyatta kutangaza kumuunga Bw Mariga, Naibu wa Rais Dkt Ruto aliwataka wanasiasa wa Jubilee kutoka mirengo ya Tangatanga na Kieleweke kujiunga na kikundi cha kampeni za mwanasoka huyo wa zamani.

Lakini wito huo wa Bw Ruto unaonekana kupuuzwa na wanasiasa wa kundi la Kieleweke.

Bw Mariga Jumatano alisindikizwa Ikuluni na Dkt Ruto, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale na Kiranja wa Jubilee Bungeni Benjamin Washiali kati ya viongozi wengineo.

You can share this post!

NYOTA PEKEE: Manchester City yafuta aibu ya Uingereza

Rais Barrow asema Gambia inakaribia kupata maridhiano

adminleo