KIKOLEZO: Utamu wa hela si hoja…
Na THOMAS MATIKO
KAMA ujuavyo, biashara ni matangazo na ndio sababu runinga nyingi huendea vichuna wenye umbo, sauti, uwezo mzuri wa kujieleza lakini hata zaidi sura zenye mvuto.
Kuonekana kwenye runinga kumewafanya wengi kuwa staa. Kwa mfano muulize Victoria Rubadiri, alipokuwa redioni Capital FM wachache mno walimfahamu.
Sio kama sasa toka alipochukuliwa na runinga ya NTV na kufanywa msomaji habari kabla ya kujiunga na Citizen TV.
Hakika kwa watazamaji wengi, kazi ya kuwa mtangazaji kwenye runinga ni kazi ya haiba na kuvutia. Kile wasichokijua ni kwamba kazi hii pia ina mapungufu yake.
Na ndio sababu mtangazaji anapoamua kuachana nayo kwa hiari, wanashindwa kumwelewa. Hawa ni baadhi tu ya watangazaji walioacha kazi hiyo inayolipa hela ndefu na kuelezea sababu zao za kutoka.
SERAH TESHNA
Serah alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Alfajiri katika runinga ya K24 hadi miezi mitatu iliyopita alipoamua kuiacha.
Akifunguka hivi majuzi, kichuna huyu anasema aliamua kuiacha sababu ilikuwa ikimchosha sana kiakili na kimwili.
“Ilikuwa inanilazimu kuamka saa tisa alfajiri ili niweze kufika studio saa 10 za alfajiri kujiandaa kwa matukio ya siku. Ni kazi iliyokuwa inanibana sana mpaka nakosa muda wa kuwa na washikaji zangu pamoja na familia,” akatiririka.
Kwa sasa anajihusisha na masuala ya utayarishaji wa vipindi na pia kazi za Mcee.
KAMENE GORO
Alikuwa mtangazaji kwenye runinga ya Ebru TV na baada ya takriban mwaka mmoja, 2017 aliamua kujitoa akisema mazingira ya kikazi pale hayangemruhusu kuendelea.
Lakini pia Kamene alisema hadi anafikia kufanya uamuzi huo, alikuwa ametimiza ndoto yake kama mtangazaji wa runinga.
“Watu hufikiri kuwa kwenye runinga ni maisha ya starehe, kuna magumu pia, sio rahisi. Hii ni mojawapo ya sababu yangu kuondoka Ebru. Lakini pia nilihitaji changamoto nyingine kwenye taaluma yangu ya uanahabari,” akasema.
Baada ya kuikacha TV, Kamene alijiunga na redio akiajiriwa na NRG kabla ya kuhamia Kiss FM.
Kwa sasa ni mmoja kati ya watangazaji wa redio maarufu zaidi. Unaweza kusema redio ndiyo iliyomfanya kuwa maarufu hata zaidi ikilinganishwa na alipokuwa kwenye runinga.
JANET MBUGUA
Baada ya zaidi ya miaka 10 akiwa mtangazaji wa runinga akifanya kazi Afrika Kusini kabla ya kuchukuliwa na Citizen TV, Janet naye aliamua kuiacha kazi hiyo.
2017 akiwa na ujauzito wake wa pili, Janet aliandikia mabosi wake barua ya kujiuzulu. Kipindi anajiuzulu, alitajwa kuwa miongoni wa watangazaji waliokuwa wakilipwa mshahara mkubwa tetesi zikidai alikuwa akipokea Sh900,000 kwa mwezi.
Pamoja na yote hayo, Janet aliamua kwenda zake huku sababu zake zikiwa alihitaji muda wa kutosha kuwa karibu na mwanawe kifungua mimba, na pia kujikita katika mambo mengine kama uigizaji. Vile vile alisema kazi ya runinga ilikuwa inamgharimu muda mwingi na pia uchovu.
KENDI ASHITIVA
Alikuwa mtangazaji wa kipindi cha Tukuza cha KTN ila baada ya miaka miwili, 2015 aliamua kuachana nayo ili kujishughulisha na programu za kuwainua kina mama.
JOEY MUTHENGI
Baada ya kukosana na mabosi wa Ebru TV kutokana na kubania mawazo yake ya utendakazi, alitua Citizen TV na ndiye mwanzilishi wa kipindi cha 10 Over 10 . Pia alikuwa na shoo ya asubuhi Day Break katika runinga hiyo.
Novemba 2018 alijiuzulu baada ya kupishana tena na mabosi wake. Kosa lake lilikuwa ni kujihusisha na utengenezaji wa tangazo la kampuni ya kubeti ya Betin kinyume na sera za Citizen TV.
Runinga hiyo inamilikiwa na kampuni ya Royal Media Services ambayo pia ndio mmiliki wa kampuni ya kubeti Shabiki. Kutokana na hilo, hakuna kampuni nyingine ya kubeti inayoruhusiwa kujitangaza kwenye runinga hiyo zaidi ya Shabiki.
Hivyo kitendo chake cha kujisakia mtonyo pale Betin kilichukuliwa kama usaliti. Mabosi wake waliamua kufanya kikao na kumwita kujieleza wakitaka achague kazi yake au Betin. Joey akachagua Betin, ishara kwamba hakuwa na nia ya kupoteza dili hiyo iliyomlipa milioni 6.
YVONNE MAINGI
Alikuwa mtangazaji chipukizi kwenye runinga ya NTV na huku nyota yake ya TV ikiwa imeanza kung’aa, aliamua kujiuzulu 2015 sababu zake zikiwa ni aweze kuendelea na masomo yake.
“Nipo kwenye hatua nzito ya masomo yangu hivyo nahitaji muda wa kutosha kuyaangazia masomo yangu na ndio sababu ya uamuzi huu,” alisema wakati huo.
Yvonne alikuwa akisomea shahada yake ya uzamifu kuhusu mabadiliko ya anga (Climate Change) katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Hajawahi kusikika tena.
ESTHER ARUNGA
Miaka 10 iliyopita, Esther alitajwa kuwa mtangazaji hodari akiwa anasoma taarifa katika runinga ya KTN.
Uhodari wake wa kujieleza na usomaji habari ulimpelekea kushinda tuzo kadhaa kama CHAT Awards 2008, iliyomtambua kuwa mtangazaji bora chipukizi.
Desemba 2010 alitangaza kuwa kajiuzulu kazi yake kwenye runinga ili kujiunga na siasa. Huo ukawa ndio mwanzo wa masaibu katika maisha yake mpaka sasa.