KIPWANI: Mzaliwa wa Congo ila kakita kambi ufuoni
Na ABDULRAHMAN SHERIFF
HUWA si jambo la kustaajabia raia kutoka DR Congo anapojitosa kwenye muziki.
Taifa hili linajulikana kwa kuchipuza vipaji vya wanamuziki ambao hutikisa ulimwengu mzima kwa mfano kina Fally Ipupa, Kanda Bongoman, Awilo Longomba na Koffi Olomide kutaja tu wachache.
Na kwa Lucas Makalamba, mzaliwa wa Butembo nchini humo, lilikuwa jambo la kawaida sana yeye kujibwaga uwanjani akiwa na umri mdogo sana wa miaka 11 na kuvutia mashabiki si haba.
Lakini ndoto ilikuwa ni kufika nchini Kenya na hasa mjini Mombasa kufanya muziki. “Kiuhakika nilishikwa na hamu kubwa ya kupiga muziki wangu katika fuo za bahari na nilichagua hasa Mombasa kwa sababu kuna mandhari za kupendeza,” asema.
Je, ndoto yako hiyo ilipotimia, ulipokelewaje?
Makalamba: Kiuhakika nimependezwa sana na jinsi nilivyopokewa na wanamuziki na mashabiki wa hapa Mombasa na kwa kipindi cha mwaka mmoja nimefanikiwa kutoa vibao vyangu vinne ambavyo vimeitikiwa vizuri.
Tupashe ni mwanamuziki wa Injili ama wa nyimbo za kidunia?
Makalamba: Mimi huimba nyimbo za Injili pamoja na za kizalendo na hasa juu ya kudumisha amani na umoja kati ya watu wa mataifa mbalimbali ya Afrika.
Ni nyimbo gani ambazo kwa wakati huu umezizindua na zinafanya vipi?
Makalamba: Ni kama vile ‘Tenda’, ‘Nisamehe’, ‘Afrika’ na ‘Mbali Nawe’. Nyimbo zilizoitikiwa zaidi ni Afrika unaozungumzia umoja wa watu wa Afrika na Mbali Nawe ambao nimegusia kuhusu maisha yangu ya zamani nilipokuwa nikitumia mihadarati na jinsi nilivyojiepusha nayo.
Ni nini tofauti ya muziki wa DR Congo na wa hapa kwetu?
Makalamba: Kusema kweli kule kwetu Congo muziki ni sawa na ibada na tuna wanamuziki wengi wazuri ila Kenya ina teknolojia bora zaidi ya kurekodi.
Unatumia mitindo gani kwa nyimbo zako na kwa sababu gani?
Makalamba: Ninatumia mitindo mbalimbali ikiwemo ile ya Rhumba, RnB, Zook na Reggae sababu inavutia vijana na tena ni rahisi kuwasilisha ujumbe.
Kuna wasanii kibao kutoka Congo waliokita kambi hapa Kenya, je, mnawasiliana?
Makalamba: Naam! Nina ukaribu sana na kina Anastazia Mkabwa, Rebecca Soki na Abigael Milonde kati ya wengine wengi.
Unasemaje juu ya muziki wa hapa nchini Kenya?
Makalamba: Vipaji vimo ila ingekuwa bora kama pia wangejifunza kucheza muziki ‘Live’ na kutumia ala kama vile gitaa, kibodi, ngoma na kadhalika.
Una malengo gani kimuziki?
Makalamba: Hamu yangu kubwa ni kufikia kiwango cha kuitwa mwanamuziki wa kimataifa. Pia ningependa kutambulika kama mwanamuziki anayehimiza uzalendo na kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.
Unapanga kurudi nyumbani?
Makalamba: Nafurahia kuwa hapa kwa sasa hasa ikizingatiwa kuwa Kenya imenikubalia kukuza kipaji changu.
Unawaambia nini mashabiki wako?
Makalamba: Nawashukuru kwa sapoti wanaoendelea kunipa.
Umewatayarishia chochote?
Makalamba: Ninawaandalia albamu ya nyimbo sita ambayo itazungumzia juu ya umoja wa mataifa yetu ya Afrika na pia kuhimiza Wakristo kutoasi dini.