• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UMBEA: Siku zote uhusiano ulioelemea upande mmoja hauwezi kufanikiwa

UMBEA: Siku zote uhusiano ulioelemea upande mmoja hauwezi kufanikiwa

Na SIZARINA HAMISI

WAPO akina dada walio kwenye uhusiano wenye miiba.

Kwamba kulia sababu ya mume imekuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Iwapo upo kwenye uhusiano ama ndoa na unajikuta kila wakati unalia, kuhuzunika ama kukosa amani, basi uhusiano huo sio wa kujenga bali wa kuangamiza.

Wapo wale wanaoishi katika utumwa wa mapenzi. Ni pale unapokuta mwanamke anaishi na mwanaume ambaye hampendi kwa moyo lakini analazimika kuwa naye kwa sababu binafsi.

Wapo pia wale wanaoishi na waume ama kuwa na uhusiano na mwanaume ambaye hana mapenzi nawe na unajua kabisa hana mapenzi nawe lakini unalazimisha ukiamini kwamba siku moja anaweza kubadili uamuzi wake.

Aina hizi mbili za utumwa ndizo zinazowasumbua wengi na kuendelea kuteseka katika uhusiano ambao mwisho wake ni matatizo.

Unapokuwa kwenye uhusiano wa aina hii, ni nadra furaha kutawala maisha yako kwani utakuwa ni mtu wa kukosa amani na kuwa mwenye fukuto la uchungu.

Halafu wale wanaoamua bora iwe, wanakuwa kwenye uhusiano ambao mmoja wao anakuwa hana mapenzi kwa mwenzake lakini analazimisha kuwa naye kwa sababu ya kupata masilahi. Mapenzi ya aina hii siku hizi yanaonekana kwa wengi.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa keshaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu, pengine pesa, mali ama heshima katika jamii.

Shida inakuja pale ambapo jamaa anapomua kufunga ndoa naye, mara nyingi anaweza kusita lakini baada ya kufikiri kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa marafiki wenye tamaa kama yeye, huamua kuingia katika ndoa na mwanaume ambaye hajampenda akitegemea kupata maisha mazuri.

Ukikutana na dada huyu baada ya miaka miwili ama mitatu ya ndoa, unaweza ukastaajabu alivyozeeka na kupoteza uang’avu wake asilia.

Uwanja wa mapenzi ni mpana sana, wakati mwingine unatakiwa kutumia akili ili uweze kung’amua ufanyacho kama ni sahihi au kama unachemsha.

Uwanja mpana wa mapenzi

Katika mapenzi kuna aina nyingi za uhusiano, wengine huwa na mtu kwa muda mfupi wakati wapo ambao wanatamani sana kuishi na wenzao baada ya kuwa katika uhusiano wa kawaida.

Inapendeza sana kama wote mtakuwa mnawaza katika umoja, yaani lililopo kichwani mwako ndilo lililomo kichwani mwa mpenzi wako, vinginevyo sio ajabu mmoja wenu akalia.

Unapokuwa katika uhusiano na mpenzi ambaye moyo wako umemfia na unatamani kufunga naye ndoa, lakini wakati huohuo mpenzi wako huyo hana muda nawe, utambue bayana kwamba unaingia kwenye shida na matokeo yake huwa sio mazuri.

Inawezekana ukawa unafahamu juu ya jambo hilo na unachojaribu kufanya ni kumlazimisha au kumshawishi zaidi ili awe na fikra kama zako jambo ambalo mara nyingi husababisha mtafaruku.

Hata hivyo siyo kila aliye katika uhusiano usio na dira anakuwa ameamua kwa ridhaa yake, wapo wanaolazimishwa na wazazi au walezi lakini pia kuna ambao hudhamiria kuwashawishi wenzao wabadili uamuzi ili mwisho wa siku waweze kuolewa.

Katika yote, uhusiano ni wa watu wawili, hata siku moja uhusiano ulioelemea upande mmoja hauwezi kuwa na mafanikio.

Inawezekana wakati mwingine tunakuwa na matumaini, kwamba huenda atabadilika, huenda atanipenda, huenda ataacha kunywa pombe, huenda atafanya hivi ama vile.

Ukiingia kwenye uhusiano na mtizamo wa aina hii, ujue kwamba furaha utaisikia kwa jirani. Kuwa makini na siku zote, kupanga ni kuchagua.

 

[email protected]

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Lau kama si kiboko, hawa hawangeitwa...

FATAKI: Piga nakshi ujuzi wa kubingirisha kamba kabla...

adminleo