Makala

DAU LA MAISHA: Alisha familia kwa kuunda majeneza

September 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

SIO wengi wanaotaka kufanya kazi au huduma zinazohusishwa na mauti.

Na hasa kwa wanawake, ni wachache ambao wako tayari kujibwaga humo kusaka riziki.

Hata hivyo kwa Rosemary Omollo, 36, mambo ni tofauti kabisa.

Mkazi huyu wa Nairobi ametupilia mbali dhana potovu na woga na kujikakamua kusaka kipato katika biashara ya kuunda na kuuza majeneza.

Yeye ni mmiliki wa Glorious Touch Funeral Services, kampuni ya kuunda na kuuza majeneza katika mtaa wa Jericho, viungani mwa jiji la Nairobi.

Bi Omollo ambaye amefanya kazi hii kwa miaka mitano sasa, hakai tu kitako kusubiri bidhaa hizi ziundwe na wafanyakazi wake, bali hata yeye akihitajika, hushika msumari na nyundo kuhakikisha kwamba mwendazake anasindikizwa kwa heshima.

“Nafahamu kazi hii yote kuanzia uunganishaji wa mbao, kuunda umbo la jeneza hadi hatua ya mwisho ya kupiga nakshi na kurembesha. Ni suala ambalo limeniwezesha kuhakikisha kwamba bidhaa zetu ni murwa kwani nina ufahamu wa kuwarekebisha mafundi pia,” aeleza.

Majeneza anayouza yako katika vitengo vinne. Kuna kitengo cha kinachohusisha majeneza sahili kabisa (Plain).

Haya huuzwa kwa kati ya Sh10,000 na Sh15, 000.

Kisha kuna kitengo cha ‘semi executive’ ambacho ni cha kiwango cha juu kidogo na yanauzwa Sh25,000 na Sh30,000. Alafu kuna kitengo cha ‘executive’ kinachohusisha majeneza ya juu ambapo yanauzwa kwa kati ya Sh30,000 na Sh 5,000. Mwisho kuna kitengo cha VIP; majeneza ya viwango vya juu zaidi sio tu kimuundo, bali pia kulingana na bidhaa zilizotumika na ni kati ya Sh50,000 na Sh70,000.

Azma yake ilichochewa na marehemu kakake ambaye tayari alikuwa anaifanya kazi hii. “Nilipojiunga na kaka yangu, nilianza kwa kushona zana za ndani za jeneza. Lakini baada ya kakangu kuaga dunia, niliamua kujitosa ndani kuziba pengo aliloacha,” asema.

Pia, anasema kwamba alijihusisha na biashara hii kutokana na kiu ya kutaka kuwahudumia vyema watu waliopatwa na msiba. “Wakati huu huwa mgumu sana kwa waliofiwa, na mambo huwa mabaya hata zaidi iwapo hawatapata bidhaa inayoambatana na thamani ya pesa zao. Nilitaka kuwa hapo kuhakikisha kwamba nawaliwaza kwa njia hii,” aeleza.

Na hajutii uamuzi wake, kwani mbali na kumpa usemi katika jamii kutokana na uwezo wake wa kujitegemea, kazi hii inamsaidia kukidhi mahitaji yake na ya familia yake.

“Kwanza kabisa tunaendesha biashara hii na mume wangu ambapo tunapata riziki ya kila siku,” aeleza.

Wateja wake ni watu kutoka ngazi mbalimbali ambapo kwa mwezi anasema anaweza kuuza kati ya majeneza matano na kumi.

Na biashara hii haimnufaishi yeye pekee kwani ana wafanyakazi 14 ambao wanamtegemea.

Lakini mambo hayajakuwa rahisi kwake kwani kama biashara zingine, pia hii haikosi changamoto.

“Changamoto ni kwamba hii sio biashara ambayo waweza lalama hadharani kuhusu ukosefu wa wateja kwani watu watakuona kana kwamba unafurahia mauti,” asema.

Pia, anasema kwamba changamoto kuu imekuwa unyanyapaa dhidi ya watu wanaohusishwa na biashara za wafu.

“Kuna baadhi ya watu wasiotaka kuhusishwa na watu kama sisi. Aidha, kunao wanaodhani kwamba sisi hufurahia kuona watu wakifa ili tupate biashara, ambapo sio ukweli,” aeleza.

Japo kwa sasa anafanya biashara hii kwa uchangamfu na bidii, anasema kwamba hata kwake mwanzoni mambo hayakuwa rahisi.

“Mimi nilikuwa naogopa sana hata kusongea majeneza, lakini baada ya kuwapoteza jamaa kadha wa karibu, ilinibidi kubadilisha mawazo yangu na kukubali kwamba hii ni biashara kama zingine na taratibu nikaanza kuzoea,” asema.

Ushauri wake kwa wanaohofia biashara zinazohusishwa na wafu ni; “kila nafsi itaonja mauti, kumaanisha kwamba kifo ni uhalisia wa maisha na hivyo hakipaswi kuogofya.”