• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Ripoti yaanika uozo ulivyokithiri katika vyuo vikuu

Ripoti yaanika uozo ulivyokithiri katika vyuo vikuu

Na OUMA WANZALA

KASHFA ya matumizi mabaya ya pesa katika Chuo Kikuu cha Maasai iliyofichuliwa majuzi, ilifunua uozo uliokolea katika vyuo vikuu vya umma nchini.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Umma imeonyesha kuwa fedha nyingi hazitumiki inavyofaa katika vyuo vikuu vya umma.

Tayari, Waziri wa Elimu Prof George Magoha ameeleza kwamba lazima vyuo vikuu vitafute njia mbadala ya kutosheleza mahitaji yake ya kifedha.

Ripoti za kifedha za vyuo vikuu vingi zinaonyesha kuwa baadhi haviwezi kutimiza mahitaji yake ya kimsingi, huku fedha nyingi pia zikitumika vibaya.

Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) kilishindwa kueleza jinsi Sh50 milioni zililipwa mwanakandarasi ambaye alitarajiwa kujenga ua kwa gharama ya Sh68 milioni ilhali mradi huo umekwama.

Vilevile, kuna maswali kuhusu Sh14 milioni ambazo zilitumika kwa ujenzi wa mradi wa kusafisha maji, ambao pia umekwama.

Ripoti ilionyesha kuwa Chuo Kikuu cha Nairobi ni kama kimefilisika, ambapo hakiwezi kukidhi mahitaji yake ya kimsingi. Kwa mfano, Chuo hicho kina madeni ya Sh5.7 bilioni, ilhali mali wanayomiliki ni ya thamani ya Sh4.2 bilioni, hilo likimaanisha kuwa lazima kipate usaidizi kutoka kwa serikali na wahisani wengine.

Ilionyesha kuwa kwa mwaka mmoja uliopita, wanafunzi wana deni lake la Sh 871 milioni.

Chuo Kikuu cha Multimedia pia kiko katika hali hiyo, kwani kilishindwa kulipa pensheni na kodi ya Sh242 milioni na Sh331 milioni mtawalia.

Chuo Kikuu cha Kisii kilishindwa kueleza jinsi kilitumia Sh230 milioni kuwalipa wahadhiri walioajiriwa kwa kandarasi, kinyume na mpango wake wa awali kutumia Sh99 milioni kuwalipa.

Hali ni kama hiyo

Hali ni kama hiyo katika vyuo vikuu vya Eldoret, Dedan Kimathi na Masinde Muliro.

“Hali ilivyo sasa, huenda vyuo vingi vikalazimika kuuza baadhi ya mali vinavyomiliki ili kulipa madeni vinayodaiwa,” alisema waziri, kwenye ripoti aliyowasilisha kwa Kamati ya Bunge Kuhusu Elimu.

Kulingana na ripoti iliyotolewa majuzi na Benki ya Dunia kuhusu hali ya elimu ya juu nchini, vyuo vikuu vinapaswa kutafuta njia mbadala za kupata fedha badala ya kutegemea ufadhili wa serikali.

Wakati huo huo, imebainika kuwa wanafunzi katika vyuo vikuu nchini wanafunzwa jinsi ya kusoma na kupita mitihani pekee badala ya kufikiria, imeonyesha ripoti hiyo.

Inaeleza kuwa utaratibu wa masomo katika vyuo vikuu nchini huwa hauzingatii masuala ya utendaji.

“Taratibu nyingi za ufunzaji ni za zamani katika taasisi nyingi za elimu ya juu. Mtaala unaotumika pia ni wa zamani na haujawianishwa na mabadiliko ya kisasa katika sekta ya elimu,” inasema.

Tayari, serikali imetangaza mipango ya kufanya mageuzi katika vyuo vikuu, ambapo baadhi vitafutiliwa mbali ama kuunganishwa.

You can share this post!

Mkewe Cohen ataka aachwe huru amzike mume

BI TAIFA AGOSTI 12, 2019

adminleo