• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Nyamweya kujibwaga uwanjani kuwania urais FKF

Nyamweya kujibwaga uwanjani kuwania urais FKF

Na JOHN ASHIHUNDU

Mwanasiasa Sam Nyamweya ameahidi kufufua soka kuanzia mashinani iwapo atachaguliwa kama rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF).

Nyamweya alisema atajibwaga uwanjani kuwania uadhifa huo baada ya Wakenya kuendelea kujiuliza masuali mengi kutokana na uongozi duni wa Rais wa sasa, Nick Mwendwa.

Nyamweya ambaye alikuwa rais wa FKF kati ya 2013 na 2016 ametangaza nia yake, muda mfupi tu baada ya aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Vihiga, Moses Akaranga kujiunga na kinyang’anyiro hicho kumpinga Mwendwa ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka mitatu tangu 2016.

Wengine waliotangaza kuwania uadhifa huo kwenye kura zitakazofanyika Desemba ni aliyekuwa mwenyekiti wa Tawi la Magharibi la Shirikisho la Ska Kenya (FKF), Andrew Amukowa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Makocha wa Soka Nchini (KFCA), Hamisi Shivachi.

Nyamweya ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FKF kati ya 1996-200 alijiondoa dakika ya mwisho kabla ya kufanyika kwa uchaguzi uliopita ameeleza kuudhishwa kwake na jinsi hali ya soka ilivyodidimia nchini kwa kiasi kikubwa.

Alisema Mwendwa hana ufahamu kuhusu soka huku akidai kwamba uchaguzi wake haukuwa huru na haki, kwani wapiga kura wengi walipokea maelezo ya kuhakikisha ameibuka mshindi.

Alisema wote waliochaguliwa kutoka kundi lao la ‘Team Change’ ya Mwendwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa sababu hawkuwa na ufahamu wowote juu ya soka.

“Wakenya walishuhudia mara kadhaa jinsi wapigaji kura walivyokuwa wakipokea maagizo ya nani wa kumpigia kura ndani kkumbi zilizofanyika uchaguzi huo kitendo ambacho si halali huku muda wa kampeni ukiwa umekwisha,” alisema Nyamweya.

“Miaka mine tangu niondoke usukani, kiwango cha soka nchini kimedidimia kwa kiwango kikubwa. Ni ukweli kwamba FKF kwa sasa haijafanya lolote la kujivunia,” aliongeza.

Alisema anapaswa kupewa nafasi kwa vile wakati wa utawala wake, soka iliimarika kuanzia ngazi ya mashinani, kinyume na siku hizo ambapo hata ligi za ngazi za chini hazina mpango.

Nyamweya aliyeshirikiana vyema na Afisa Mkuu Michael Esakwa alisema wakati wake alifanikiwa kupata ufadhili kutoka kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) ambao ulitumiwa kuukarabati uwanja wa Moi Stadium, Kisumu na Nairobi City Stadium mbali na ujenzi wa kituo cha Goal Project.

Wakati huo, alisema Kenya ilipata fursa ya kuandaa mafunzo ya bara kwa wakufunzi wa soka-Caf C Coaching Licence ambapo waliofaulu walipokea vyeti vya ukufunzi.

Nyamweya vile vile alikumbuka alivyofanikiwa kupata wadhamini wa Supa Ligi, kinyume na ilivyo sasa ambapo timu hizo zinasumbuliwa kutokana na matatizo ya kifedha. Udhamini huo ulichangia upinzani mkali miongoni mwa timu zilizoshiriki.

“Wakati wangu, waamuzi walilipwa kwa wakati, kinyume na ilivyo sasa. Kwa mfano Supa Ligi ambayo inakutanisha timu 20 imeanza huku zikilia kwamba huenda zikavurugwa na matatizo ya kifedha,” alisema.

Alipeana mfano wa Vihiga United ambayo ilipanda ngazi hadi KPL mnamo 2017, miaka mine tu baada ya kubuniwa, lakini ikashuka haraka kutokana na matatizo ya kifedha.

Mount Kenya FC ambayo iliteremshwa ngazi msimu uliopita, haijajirekebisha pia bada ya kukosa mdhamini.

Awali, chini ya Nakumatt Holdings, timu hii ilikuwa tishi kwa timu kubwa kabla ya kubadilisha jina.

Chini ya usimamizi wa mwanasiasa Francis Mureithi, timu hii ilipeana pointi za bwerere kwa klabu ya Gor Mahia na Mathare United.

Kwa upande mwingine, Shabana FC imejipata katika mashaka kama hayo na tayari viongozi wake wameanza kulia baada ya kulemewa kugharamia mahitaji ya wachezaji.

Iwapo Nyamweya atatoa mafesto yake na kueleza vizuri atakapotoa ufadhili wa kudhamini klabu zetu za Ligi Kuu ya Kenya (KPL), za Supa Ligi pamoja na waamuzi, soka yetu itaimarika kwa kiwango kikubwa.

You can share this post!

Arsenal, Manchester United nari katika Uropa

Mudavadi hahitaji ‘baraka’ za Raila 2022, ANC yasema

adminleo