• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
Nuksi zaandama Wanyama akirejea uwanjani, Spurs yalimwa na Leicester

Nuksi zaandama Wanyama akirejea uwanjani, Spurs yalimwa na Leicester

Na GEOFFREY ANENE

VICTOR Wanyama alirejea uwanjani kwa mikosi baada ya kukosa mechi 11 zilizopita, huku Tottenham Hotspur ikipigwa 2-1 na Leicester City uwanjani King Power kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza, Jumamosi.

Kiungo huyo Mkenya, ambaye Spurs haikufaulu kumuuza katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichofungwa barani Ulaya mnamo Septemba 2, alisababisha Leicester kusawazisha alipopiga pasi fyongo ambayo hatimaye ilifungwa na Ricardo Pereira dakika ya 69.

Harry Kane alipeleka Spurs mapumzikoni kifua mbele 1-0 baada ya kufunga bao safi akiwa sakafuni kutokana na pasi ya Son Heung-min dakika ya 29.

Dakika mbili baada ya Wanyama kujaza nafasi ya Moussa Sissoko katika dakika ya 67, Pereira aliona lango kutoka na pasi ya Wanyama kukosa kufikia mchezaji wake.

James Maddison alifungia Leicester bao la ushindi dakika ya 85 kutoka nje ya kisanduku, pia Wanyama akiwa karibu. Wanyama hakuwa na bahati kwa sababu pia alilishwa kadi ya njano dakika nne tu baada ya kuingia uwanjani kwa kucheza visivyo.

Itakumbukwa kuwa kabla ya Leicester kupata bao la kwanza, Spurs ilikuwa imefunga bao la pili kupitia kwa Serge Aurier dakika ya 65, lakini likafutiliwa mbali na teknolojia ya VAR kwa kuotea.

Kichapo hiki ni cha kwanza cha Spurs mikononi mwa Leicester ambayo ilikuwa imepoteza mara tatu dhidi ya wapinzani hawa.

Ushindi umewezesha Leicester ya kocha Brendan Rodgers kurukia nafasi ya pili kwa alama 11, alama nne nyuma ya viongozi Liverpool watakaoshuka uwanjani kuzichapa dhidi ya Chelsea mnamo Jumapili. Spurs ya kocha Mauricio Pochettino ni ya tano kwa alama nane.

You can share this post!

Gladys Wanga aelezea jinsi Ida Odinga alivyomsaidia...

Jubilee yaelezea uwezekano wa kumwadhibu Kamanda

adminleo