• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Madiwani wa Mandera watoa ahadi kupitisha ‘Punguza Mizigo’

Madiwani wa Mandera watoa ahadi kupitisha ‘Punguza Mizigo’

Na MANASE OTSIALO

MADIWANI wa bunge la Kaunti ya Mandera, Ijumaa waliahidi kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance, Ekuro Aukot, kwamba wanaunga mswada wake wa kubadilisha katiba wa ‘Punguza Mizigo’.

Wakiongozwa na Naibu Spika, Farah Abdi Abdinoor, madiwani hao walisema kwamba waliridhishwa na mswada huo baada ya kukutana na Bw Aukot.

“Tulikutana na Dkt Aukot na kundi lake na wakajibu maswali yetu yote tukaridhika. Tutafuata utaratibu unaofaa kutekeleza jukumu letu,” alisema Bw Abdinoor.

Mwenyekiti wa kamati ya sheria ya bunge hilo Mohamed Ibrahim Yusuf alihakikishia umma kwamba madiwani watashughulikia mswada huo.

“Tunaendelea kupokea maoni kuhusu mswada huo na tutafuata utaratibu unaofaa ikiwa ni pamoja na kuwasilishwa mbele ya kikao cha bunge la kaunti,” alisema.

Diwani wa wadi ya Rhamu, Kullow Alio Guyow, alisema wakazi wa Mandera watawakilishwa kabla ya kuamua hatima ya mswada huo.

Kupunguza viti

Kwenye kikao cha umma Ijumaa, wakazi walihimiza madiwani kukataa mswada huo wakidai unapunguza viti vya uwakilishi.

Kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hiyo Bw Abdi Adan Ali, alisema mswada huo utaidhinishwa ikiwa unalinda ugatuzi na kuhakikisha kaunti zitatengewa pesa zaidi.

“Tunachotaka ni kulinda na kuimarisha ugatuzi,” alisema.

You can share this post!

Wafanyakazi wakerwa na KPA kuuza nyumba

Bilionea Punjani arejea nchini kisiri

adminleo