MWANASIASA NGANGARI: Gichuru, mzalendo aliyeibuka mwiba kwa wakoloni
Na KENYA YEAR BOOK
HISTORIA ya taifa hili haiwezi kuandikwa bila jina la James Samuel Gichuru, Waziri wa kwanza wa Fedha baada ya Kenya kujinyakulia uhuru, msomi na mwanasiasa mahiri ambaye alishabikiwa sana kutokana na uzalendo wake.
Marehemu Gichuru – wakati wa uhai wake – alijizolea sifa kama kiongozi ambaye aliweka mbele maslahi ya taifa kwa kupigania uhuru na pia anakumbukwa kama mwandani na rafiki mkubwa wa mwanzilishi wa taifa hili hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Gichuru alizaliwa 1914 kwa Samuel Gitau na Mariam Nyaguthi katika eneo la Thogoto, Kikuyu, Kaunti ya Kiambu na alikuwa mwana wa kwanza kwenye familia iliyojaaliwa watoto tisa.
Akiwa katika familia ambayo ilikuwa ya kumcha Mungu kutokana na kuwasili kwa Wamishenari ambao walijenga makanisa na shule kadhaa eneo la Kikuyu, Gichuru na watoto wenzake walilazimika kutii amri ya wazazi wao na kutilia manani masomo yao hasa ikizingatiwa kwamba marika wake wakati huo walikuwa wakiwachunga mifugo na kushiriki tamaduni mbalimbali za jamii ya Agikuyu.
Kutokana na uhusiano mzuri kati ya wazazi wake na Wamishenari hao, Bw Gichuru alipata nafasi ya kujiunga na Shule ya Kimish nari ya Kikuyu kwa masomo ya shule ya msingi kisha akajiunga na Shule ya Upili ya Alliance alikomaliza masomo yake akiwa na umri wa miaka 16.
Gichuru kisha alielekea katika Chuo Kikuu cha Makerere na kufuzu na stashahada kwenye kozi ya ualimu.
Kati ya mwaka wa 1935 na 1940, alirejea kufundisha Alliance ambapo walimu wake wengi walikuwa Wazungu na akaungana na mpiganiaji uhuru na mojawapo wa mawaziri wa kwanza katika serikali ya Mzee Kenyatta, J D Otiende ambaye pia alikuwa mwalimu shuleni humo.
Kulingana na dadake Hannah Wanjiri ambaye mwaka 2019 alitimu umri wa miaka 90, Gichuru alikuwa na msukumo wa kuhakikisha Waafrika wote wanapata elimu akiwa mwalimu.
Kati ya waliokuwa wanafunzi wake shuleni Alliance ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Charles Njonjo na nduguze waziri wa zamani Njoroge Mungai, wanaofamika kama Nyoike na Ng’ethe.
Sifa za uanaharakati za Gichuru zilianza kuonekana akifundisha Alliance ambapo alipinga sheria nyingi za kikoloni mojawapo ikiwaamrisha walimu Waafrika kuvalia suruali iliyofanana na sare ya wanafunzi huku walimu Wazungu wakivaa suruali ndefu.
Alipata jiko mwaka wa 1936 akiwa bado anafundisha Alliance na pamoja na Rahab Wambui Ndatha, walijaaliwa watoto wawili. Ndatha pia tayari ni marehemu.
“Alliance ilikuwa shule ya Wazungu na Waafrika walilazimishwa kuwaiga. Hata hivyo, Gichuru alikiuka na kuanza uanaharakati wa kupigania uhuru alipogundua kwamba sera za Wazungu zilikuwa zikiwanyanyasa Waafrika ambao hawakuwa na hatia,” akasema Wanjiru.
Gichuru alijitosa rasmi kwenye uwanja wa kisiasa mwaka wa 1940 na mara kwa mara aliendesha baiskeli yake hadi maeneo ya mbali ili kukutana na viongozi wengine wazalendo ambao walikuwa na kiu ya kumwona Mwaafrika akijitawala na kujiamulia maisha yake.
Alichaguliwa Mwenyekiti wa Kenya African Union (KAU) 1944, wadhifa ambao aliuachia Mzee Kenyatta 1946, baada ya Mzee kurejea kutoka Uingereza alikoenda kusoma.
Hata hivyo, historia hiyo ilijirudia 1961 alipojiuzulu cheo chake kama Rais wa chama cha Kenya African National Union (Kanu) na kumkabidhi Mzee Kenyatta wadhifa huo baada yake kuwachiliwa huru kutoka gerezani.
“Alitumia wadhifa wake alipokuwa mwenyekiti wa Kanu kupigana na utawala wa wakoloni na kuwaunga mkono wapiganiaji wa Mau Mau. Alienda hatua moja zaidi kuwatuma walinzi aliopewa na wakoloni kulinda maeneo ambayo wapiganiaji hao walilishwa kiapo.
Mara nyingi alikuwa akiandaa mikutano mingi vijijini na kuwaambia Waafrika kwamba siku za mkoloni zilikuwa zimehesabiwa nchini,” akaongeza dadake.
Ilipofika mwaka wa 1953, Wazungu walichoshwa na tabia zake za kuwachochea Waafrika ndipo akatiwa mbaroni baada ya kuongoza mkutano wa umma kwenye soko la Dagoretti.
“Wanawake wamejifungua wanaume wengi lakini mamangu alijifungua mpiganiaji halisi,” alisema kwenye mkutano huo uliotajwa kama wa uchochezi.
Ni kutokana na matamashi hayo ambapo mkuu wa wilaya wakati huo alifika nyumbani kwake Thogoto siku mbili baadaye akiwa ameandamana na maafisa wa polisi kisha akanyakwa na kuingizwa kwenye lori kisha kusafirishwa hadi Githunguri.
“Babangu alibebwa juu hobelahobela na kuingizwa kwenye karadinga na tulikosa kumwona kwa miaka kadhaa baadaye,” anakumbuka bintiye, Njoki Ndungi.
Gichuru aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani Githunguri kisha baadaye akahamishwa katika eneo la Gatamaiyu wakoloni walipogundua kwamba alikuwa na jamaa na marafiki waliomtembelea Githunguri na kumtia moyo ili aendeleze vita dhidi yao.
Kati ya 1953 hadi 1961, Gichuru aliibuka kiongozi shupavu ambaye alishirikiana na Jaramogi Oginga Odinga, Tom Mboya, Mzee Kenyatta, Paul Ngei, Bildad Kagia na mashujaa wengine kupigania uhuru wa taifa kwa kukataa uongozi wa kiimla wa wakoloni na kuwashinikiza warejee kwao.
Kwa mfano, mapema 1961 alilazimisha serikali ya kikoloni kumwaachilia Mzee Kenyatta kutoka gerezani kisha akashinikiza sheria ibadilishwe ili aruhusiwe kujiunga na Bunge la Legco, akisema kiongozi huyo hakuwa hatari kwa usalama wa nchi jinsi wakoloni walivyowataka raia waamini.
Baada ya kuteuliwa waziri wa fedha na Mzee Kenyatta 1963, Gichuru alizamia miradi ya kuimarisha maisha ya Wakenya kwa kuanzisha Benki ya kwanza ya Waafrika (ADB) na kuhakikisha Wakenya wanagawiwa vipande vikubwa vya ardhi vilivyoachwa na wakoloni.
Katika miaka ya mwisho ya utawala wa Mzee Kenyatta, Gichuru alihamishwa hadi wizara ya Ulinzi, cheo alichoshikilia hata baada ya Daniel Arap Moi kuchukua usukani 1978.
Aliaga dunia 1982 baada ya kuugua kwa muda mrefu, mwaka huo akiwa bado akihudumu kama mbunge wa Limuru.