Kadhia ya mifugo mijini itaendelea hadi lini?
Na SAMMY SAWERU
WIKI moja baada ya Taifa Leo kuangazia suala la ng’ombe wanaoachiliwa kujitafutia lishe katika baadhi ya mitaa kaunti ya Nairobi kuhangaisha wafanyabiashara na wakazi, wamiliki kadhaa wa mifugo hao wamejitokeza na kujitetea vikali.
Mitaa iliyotajwa – hasa wafanyabiashara wa bidhaa za kula kuhangaishwa – ni Roysambu, Zimmerman, Githurai na Carwash.
Kwa mujibu wa wamiliki wa ng’ombe tuliozungumza nao, wanadai huwa wamekodishwa mahala pa kulishia mifugo wao.
“Mimi ni Mkenya anayeheshimu watu na sheria. Siwezi ingiza ng’ombe katika shamba au ploti ya mtu bila ruhusa. Tunakowalishia huwa tumekodishwa,” akasema mmiliki tuliyekutana naye eneo la Zimmerman akiendelea kuchunga mifugo yake.
Baadhi ya wafanyabiashara wanalalamika kuwa ng’ombe wanaozunguka kiholea eneo hilo wanawasababishia hasara ya bidhaa wanazouza kama vile mboga, matunda na nafaka.
Mchungaji mwingine naye alijitetea kwamba yeye ni makini katika kufuata ng’ombe wake na kwamba hajawahi kuhusika katika cha kuwaachilia wale bidhaa za watu.
“Sijasikia yeyote akinilalamikia kwa sababu mimi huwa makini,” akasema.
Wakazi wa maeneo yanayotajwa kuathirika wana malalamiko tele wakidai ng’ombe hao wamekuwa kero kuu. Mkazi wa Zimmerman na ambaye pia mkulima amesema kwamba wiki tatu zilizopitia mboga zake shambani zilitafunwa na ng’ombe.
Licha ya kufahamisha aliyekuwa nao, hakufidiwa.
“Wenye ng’ombe hawajali kamwe. Mifugo hiyo imekuwa tishio hata kwa watoto, kuchafua mazingira na kuingia katika maboma na ploti za watu,” akasikitika.
Imebainika kuwa baadhi ya ng’ombe wanatoka eneo la Kiserian, Ruai na Kitengela. Aidha, pia wamekuwa kero kwa watumizi wa barabara kwani hutatiza shughuli za usafiri na uchukuzi wanapofuka.
Ni jukumu la serikali ya kaunti ya Nairobi, hasa wizara ya kilimo na mazingira pamoja na halmashauri ya kitaifa ya mazingira, Nema, kuingiliala kati suala hili na kutafuta suluhu.
Awali, mbunge mwakilishi wa wanawake wa Kiambu katika Bunge la Kitaifa, Gathoni Wa Muchomba alikuwa ametangaza kuwa atawasilisha mswada bungeni kuangazia suala la ng’ombe kuhangaisha wakulima Kiambu na Nairobi.