Sheria mpya ya gesi kisiki kwa wafanyabiashara
Na LAWRENCE ONGARO
SHERIA mpya ya uuzaji wa mafuta na gesi imelazimisha wafanyibiashara wengi kufunga biashara zao Murang’a.
Mamlaka ya kudhibiti bidhaa hizo imezindua notisi nambari 99 na 100 ya kudhibiti bidhaa hizo jambo ambalo limeleta tumbo joto kwa wafanyabiashara wengi.
Miji iliyoathirika kwa sasa ni Kabati, Gatanga, na Kenol katika Kaunti ya Murang’a.
Kaunti ambazo zinafuata maagizo hayo zimeanza kukabiliana na wafanyi biashara wanao kiuka sheria hiyo.
Barua iliyowasilishwa kutoka kwa wizara ya ndani kwa makamishna wote wakuu imetoa amri wabuni jopo la maafisa kadha litakalo wanasa wale wote wanaoendesha biashara hiyo ya gesi bila kufuata sheria mpya iliyowekwa na idara hiyo ya (LPG).
Sheria hiyo mpya inahitaji wafanyi biashara hao wa kuuza mitungi ya gesi kukata leseni mpya na kufuata sheria zote zilizowekwa.
Kulingana na wizara ya uchimbaji wa madini na petroli ya notisi nambari 99 na 100 ni sharti ijulikane vyema aina ya mitungi za gesi zinazobadilishwa kwenye vituo tofauti ni bora.
Uchunguzi uliyofanywa katika maeneo tofauti imebaini ya kwamba vituo vingi vya kuuza mitungi za gesi vimefungwa kutokana na sheria hiyo mpya.
Bi Mary Wangui kutoka mji wa Kabati kaunti ya Murang’a, anasema kwa sasa ameacha biashara hiyo kwa muda na kuingilia uuzaji wa makaa.
“Tunaiomba serikali kuwapa watu muda wa kutosha ili wajipange. Sheria mpya iliyoletwa ni kali sana,” alisema Bi Wangui.
Mkazi mmoja wa Kandara mkewe na wafanyi kazi wengine walitiwa nguvuni juzi ijumaa kufuatia sheria hiyo mpya.
Wengi wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya kukiuka sheria hiyo na kuachiliwa kwa dhamani ya Sh 50,000 huku wakingoja kuendelea na kesi.
Bw Nyaga Gichuru ambaye pia ni mfanyi biashara anasema anajitayarisha kupata leseni mpya lakini anaiomba serikali kuwapa muda ili nao wajipange.
Inadaiwa msako huo utaendelea kote nchini, jambo ambalo litasababisha upungufu wa gesi nchini na pia kupanda kwa bei yake.
Uchunguzi umebainisha kuwa kuna vituo kadha maeneo mengi ambazo zinaendeleza biashara ya kujaza gesi kwenye mitungi jambo ambalo ni hatari kufuatia ukaguzi wake kabla ya kupeleka vituoni.