• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
Wanafunzi wa Precious kuhamishiwa shule mpya

Wanafunzi wa Precious kuhamishiwa shule mpya

Na VALENTINE OBARA

SERIKALI itaamua mahali ambapo wanafunzi wa Shule ya Precious Talent wataendeleza masomo yao ifikapo Jumatatu.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha jana alisema shule hiyo itafungwa kwa sasa.

“Kufikia Jumatatu tutakuwa na ripoti ya wataalamu watakaotushauri kama wanafunzi watahitajika kuhamishwa shule nyinginezo zilizo karibu,” akasema Prof Magoha.

Baadhi ya wanafunzi walikuwa wakijiandaa kwa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) utakaofanywa mwezi ujao na ilisemekana walifanyiwa maombi maalum wikendi.

Naibu Rais, Dkt William Ruto alitangaza serikali imetenga jumla ya Sh20 milioni ili shule ya msingi ya umma ijengwe katika ardhi inayomilikiwa na Shule ya Upili ya Lenana, kuhudumia watoto wa wadi hiyo.

Kwenye taarifa aliyotoa baada ya kutembelea watoto waliojeruhiwa ambao walikuwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Dkt Ruto alisema serikali ilifahamu mapema hapakuwa na shule ya umma katika wadi hiyo na juhudi zilikuwa za ujenzi zinaendelezwa.

Hata hivyo, mkasa ulitokea kabla ujenzi huo kufanywa.

Alisema Sh10 milioni zitatumiwa kwa ujenzi wa shule haraka na Sh10 milioni nyingine zitapeanwa kwa Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) ya eneobunge hilo la Dagoretti.

Kulingana na Dkt Ruto, inatarajiwa shule hiyo mpya itakamilika ifikapo Januari mwaka ujao na itakuwa chini ya usimamizi wa Shule ya Upili ya Lenana.

You can share this post!

Aibu ya viongozi kulaumiana baada ya mkasa wa Dagoretti

Shule nyingi za kibinafsi mabandani ni duni

adminleo