Shule nyingi za kibinafsi mabandani ni duni
Na SAMMY KIMATU
MKASA uliotokea jana katika Shule ya Precious Talent, eneobunge la Dagoretti umeibua mdahalo kuhusu hali ya elimu katika mitaa ya mabanda.
Huku ikiwa ni haki ya kila mtoto kupata elimu na kwa mujibu wa sheria za Kenya, kila mzazi hutaka watoto wake wasomee katika shule yenye hadhi ya juu.
Ni kwa msingi huu ambapo wazazi wengi huamua kupeleka watoto wao katika shule za kibinafsi.
Lakini imebainika shule nyingi za kibinafsi katika mitaa ya mabanda hupuuza mahitaji ya kimsingi kwani karo wanazolipisha pia ni za chini kwa kiwango kinachoweza kugharamiwa na wakazi wa mitaa hiyo.
Katika Kaunti ya Nairobi pekee, kuna shule nyingi za kibinafsi zilizo na miundomsingi duni mitaa ya Mukuru, Mathare, Kawangware, Kibera, Kariobangi na kwingineko.
Hali hii si tofauti katika mitaa mingine ya mabanda kota nchini.
Katika mitaa ya mabanda ya Mukuru kwenye maeneo bunge matatu yakiwemo Embakasi Kusini, Starehe na Makadara, kuna mseto wa shule za kibinafsi za chekechea, za msingi na pia za upili.
Baadhi ya shule za kibinafsi zimejengwa kwa njia inayoonyesha wamiliki wana kiu cha kujitajirisha bila kujali hali ya usalama wa wanafunzi. Shule hizo hazina hata viwanja vya kuchezea wala kuwa na bendera.
Vilevile, madarasa hayo hugeuzwa kuwa makanisa ifikapo wikendi kama njia ya wamiliki kuendeleza mapato yao.
Wakati mwingi, shule hizi huwa zimejengwa kwa vifaa duni ikiwemo mabati na tope, huku zingine zikiwa ni nyumba za zamani ambazo zimegeuzwa kuwa shule.
Hii ni kumaanisha, baadhi ya nyumba hizo zilizogeuzwa shule hazina mahitaji muhimu yanayohitajika kama vile vyoo vya kutosha.
Zile chache zilizo katika hali bora huwa zimefadhiliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali au za kidini zilizo na ufuasi mkubwa kimataifa.
Ni bayana kwamba, wakati mwingi kipaumbele kuhusu shule duni hupeanwa kwa maeneo ya mashambani lakini kuna hali mbaya zaidi katika mitaa ya mabanda mijini.