Habari

Vijana walioiba viti vya Ruto wanyakwa

September 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

STEPHEN ODUOR na HAMISI NGOWA

POLISI katika Kaunti ya Tana River wamewatia nguvuni vijana wanne kwa tuhuma za wizi wa viti katika sherehe.

Kulingana na naibu kamanda wa polisi, Tana Delta Moffat Mang’era, vijana hao waliiba viti ambavyo vilikuwa vimekabidhiwa vikundi vya akina mama wajane na Naibu Rais William Ruto, katika hafla iliyofanyika mjini Minjila, Tana Delta.

Bw Mang’era alieleza kuwa punde tu baada ya sherehe hiyo kukamilika, vijana hao waliamua kujilipa kwa kazi waliyofanya mchana ule, baada ya mwajiri wao kukosa kuwashughulikia jinsi walivyokubaliana.

“Walipewa kazi na mwakilishi wa akina mama bungeni, Rehema Hassan, ila akasahau kuwalipa kama walivyokubaliana na wao wakaamua kuiba vifaa vile,” alisema.

Alieleza kuwa afisi ya Bi Rehema iliitisha usaidizi wa polisi punde walipofahamishwa kuwa vijana hao walikuwa wametoweka na baadhi ya viti.

Ilichukua siku tano kuwasaka vijana hao kupitia kwa njia ya mtandao, ambapo nambari zao za simu zilifuatiliwa na hatimaye wakashikwa wakiwa wangali na vifaa hivyo.

Mmoja wa vijana hao hata hivyo alijisalimisha pamoja na viti alivyoiba akiomba kusamehewa kwa kosa alilolifanya.

Tukio hilo limewahuzunisha wakazi wa eneo la Tana Delta, huku wakidai kuwa baadhi ya viongozi walikuwa na mazoea ya kuwatumia vijana na kukataa kuwalipa.

Wakazi hao wamemtaka Bi Rehema kuamrisha kuachiliwa kwa vijana hao upesi na badala yake ashughulikie malipo yao kama walivyokubaliana.

Kwingineko, polisi katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa jana walikuwa macho wakati wa mazishi ya Abdalla Swaleh aliyefahamika kwa jina la utani ‘Vumbi’ aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi Jumapili alasiri.

Swaleh aliuawa alipojaribu kumshambulia afisa wa polisi kwa panga.

Jana wakati wa mazishi ya mshukiwa huyo, maafisa wa polisi walionekana wakitumia magari kushika doria katika mitaa tofauti ya eneo hilo kuepusha wenzake kulipiza kisasi kwa umma kama ilivyo desturi yao.

Kinyume na siku za kawaida, idadi ya polisi walioshika doria ilionekana kuongezeka hususan katika mitaa ambayo inaaminika kuwa maficho ya wahalifu.

Kando na wale waliokuwa wakitumia magari, pia kulikuwa na kikosi maalum kilichotumia pikipiki kupenya hadi sehemu zenye vichochoro.

Kamanda wa polisi eneo hilo Bw Benjamen Rotich alisema: “Tunajua ni kawaida vijana katika eneo hili kuzua fujo na kushambulia watu wanapomaliza mazishi ya mwenzao kwa kisingizo cha kulipiza kisasi. Tumeweka maafisa wa kutosha wa kukabiliana na tukio lolote la kuvuruga amani.”

Mshukiwa alidaiwa alikuwa katika genge la vijana sita waliokuwa wamejihami kwa panga na visu wakihangaisha wakazi wakati polisi waliokuwa wakishika doria eneo hilo walipokabiliana nao.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi eneo hilo Bw Benjamen Rotich washukiwa wengine watano walifanikiwa kutoroka wakiwa na majeraha ya risasi.

Bw Rotich aidha alisema mshukiwa alikuwa miongoni mwa washukiwa wakuu ambao wamekuwa wakisakwa na polisi kwa kujihusisha na visa tofauti vya uhalifu katika eneo la Majengo Mapya pamoja na Jamvi la Wageni na maeneo ya Bofu.